Mahakama ya biashara Marekani yazima ushuru mpya wa Trump
29 Mei 2025Mahakama ya biashara ya Marekani imezuia rasmi utekelezaji wa ushuru mpya uliopendekezwa na Rais Donald Trump dhidi ya bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nchi zinazoingiza zaidi Marekani kuliko inavyouza, ikisema amepitiliza mamlaka yake ya kisheria. Ikulu ya White House imesema itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Mnamo Aprili, Trump alitangaza ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa nyingi kutoka nje, huku akisitisha ushuru huo kwa baadhi ya nchi washirika kwa muda wa siku 90. Ushuru huo sasa unapangwa kuanza kutekelezwa Julai 8. Kwa miezi ya hivi karibuni, Trump pia ameongeza ushuru wa asilimia 25 kwa magari, chuma na alumini, na hata ushuru wa asilimia 100 kwa filamu kutoka nje.
Mpango wa Trump unalenga kuweka ushuru wa aina moja kwa bidhaa zote zinazoingia Marekani kutoka mataifa yote. Timu yake ya uchumi imeagizwa kuweka mikakati ya ushuru wa kulipiza kwa mataifa yote yanayotoza ushuru kwa bidhaa za Marekani au kutumia vizingiti visivyo vya ushuru kama masharti ya usalama wa magari au kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Nchi maalum zinazolengwa
Mexico na Canada: Mexico na Canada zikiwa washirika wakuu wa kibiashara wa Marekani mwaka 2024, zimewekewa ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa nyingi na asilimia 10 kwa bidhaa za nishati kutoka Canada kuanzia Machi 4.
Canada imeripoti kulipiza kwa ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 22. Viongozi wa Marekani wamesema mazungumzo bado yanaendelea kufikia makubaliano kwa sehemu, hususan kuhusu usafirishaji haramu wa madawa ya fentanyl.
China: Tangu Februari, Marekani imeweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zote kutoka China, ukiongezwa hadi asilimia 54 mwezi Aprili, hali iliyozua hatua za kulipiza kutoka Beijing. Hadi kufikia Mei 12, mataifa hayo mawili yalifikia makubaliano ya muda mjini Geneva, kupunguza ushuru kwa asilimia 30 na 10 mtawalia kwa kipindi cha siku 90.
Umoja wa Ulaya: Trump ameyataka mataifa ya Umoja wa Ulaya, EU, kupunguza pengo la biashara au kuagiza mafuta na gesi zaidi kutoka Marekani. Tangu Aprili 9, bidhaa nyingi kutoka Umoja wa Ulaya zimekumbwa na ushuru wa asilimia 25 hadi 50, likiwemo sekta ya magari na dawa. EU imetangaza kulipiza kwa ushuru wa Euro bilioni 26, huku mazungumzo yakitarajiwa kuendelea hadi Julai 9.
Makubaliano ya pande mbili na Uingereza
Mnamo Mei, Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmerwalitangaza makubaliano ya kibiashara yenye masharti nafuu. Mkataba huo umeacha ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za Uingereza, huku ukiweka nafuu kwa bidhaa za kilimo na magari, lakini haukushughulikia kodi ya huduma za kidigitali ya Uingereza ambayo Marekani imekuwa ikiikosoa.
Sekta zilizolengwa moja kwa moja: Bidhaa na sekta maalum pia zimeathirika au kusamehewa, zikiwemo chuma, magari, vifaa vya kielektroniki, semikondakta, dawa, mbao, na bidhaa za filamu. Ushuru mpya unaangazia maeneo ya viwanda ambako Marekani imekuwa ikikabiliana na ushindani mkali kutoka nje.