Mahakama: Mashahidi wa kesi ya Lissu kufichwa
18 Agosti 2025Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru mashahidi katika kesi ya uhaini dhidi ya Lissu kufichwa ikieleza kuwa licha ya sheria kuruhusu mwenendo wa mahakama kuwa wa wazi lakini ni haki ya mashahidi kulindwa. Kadhalika mahakama hiyo imekataza kuchapisha, kunakili na kusambaza ushahidi unaoweza kufichua utambulisho au sifa za mashahidi katika kesi hiyo.
Uamuzi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu, tayari umetolewa na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga ukiamuru kufichwa kwa mashahidi katika kesi ya uhaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Awali, Mahakama hiyo ilipokea ombi la pingamizi la kurusha moja kwa moja mwenendo wa shauri hilo juu ya sakata la utambulisho wa mashahidi raia wa kawaida.
Jumatatu, Hakimu Kiswaga ametoa uamuzi huo huku akisisitiza kuwa mshtakiwa atapewa nafasi kamili ya kusikiliza muhtasari wa mashahidi na atakuwa na haki ya kuwasilisha maombi yoyote na kusikilizwa kwa usawa.
Vyombo vya habari vyaonywa juu ya kuchapisha taarifa za mashahidi
Kadhalika mahakama hiyo imeamuru kuwa mtu au chombo cha habari kitakachokiuka maagizo ya Mahakama Kuu kwa kurusha au kuchapisha taarifa na nyaraka zinazohusu mashahidi waliolindwa, kitachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
Awali kabla ya kesi hiyo kuanza, kuliibuka mvutano mkubwa kati ya wanachama wa CHADEMA na maofisa wa mahakama baada ya CHADEMA kudai kuna polisi waliovaa kiraia wamejaza nafasi ambazo CHADEMA huketi kila wakati shauri hilo linapotajwa.
Lissu alishtakiwa kwa makosa ya uhaini na usambazaji wa taarifa za uongo mnamo Aprili mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu nchini humo imetupilia mbali ombi la CHADEMA la kutaka kuendelea na shughuli zake za kisiasa baada ya mahakama kuzuia shughuli za kisiasa za chama hicho katika kesi iliyofunguliwa na makada na viongozi wa CHADEMA walioishtaki CHADEMA kwa matumizi mabaya ya rasilimali yasiyo na uwiano kati ya Zanzibar na Bara.