Mahakama ya UN yaanza kusikiliza kesi dhidi ya Israel
28 Aprili 2025Mahakama hiyo inasikiliza kesi hiyo kuangazia wajibu wa Israel katika kufikishwa kwa msaada wa kibinadamu unaohitajika haraka kwa raia wa Palestina walioko kwenye maeneo yanayokaliwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, hata hivyo ameitaja kesi hiyo kama sehemu ya "ukandamizaji wa kimfumo na kuliharamisha" taifa lao.
Akizungumza mjini Jerusalem wakati kesi hiyo ikianza mjini The Hague, Saar amesema mahakama hiyo imekuwa ya kisiasa, na kuitaja kesi hiyo kuwa ni "aibu".
Kesi hiyo itakayosikilizwa kwa wiki nzima, inafuatia ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwishoni mwa mwaka jana, lililoiomba mahakama hiyo ya kimataifa hiyo kupima majukumu ya kisheria ya Israel baada ya kulizuia shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina kufanya kazi kwenye eneo lake.