Ujerumani yamhukumu Daktari wa Syria aliyewatesa wapinzani
17 Juni 2025Mahakama moja nchini Ujerumani hapo jana ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa daktari wa Syria ambaye aliwatesa wapinzani wa aliyekuwa mtawala Bashar al-Assad wakati wa vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Mahakama ya juu zaidi mjini Frankfurt ilimpata na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu daktari Alaa Mousa, aliotenda alipokuwa akifanya kazi kama daktari katika hospitali za kijeshi huko Homs na Damascus kati ya 2011 na 2012.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Christoph Koller alisema vitendo vya Mousa vilikuwa sehemu ya hatua za kikatili za utawala wa kidikteta wa Assad na usio wa haki.
Ujerumani imewashitaki wafuasi kadhaa wa Assadchini ya kanuni ya "mamlaka ya kimataifa", ambayo inaruhusu uhalifu mkubwa kushtakiwa hata kama ulitendwa katika nchi tofauti.