Mahakama ya ICJ kukamilisha kesi kuhusu Israel
2 Mei 2025Maoni yatakayotolewa na majaji 15 wa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa yatatumiwa kama mwongozo wa kisheria kwa vyombo mbalimbali duniani.
Mahakama hiyo ya kimataifa ya Haki ICJ, ilianzisha keshi hiyo baada Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuitaka mwaka jana kutoa maoni yake juu ya wajibu wa kisheria wa Israel kufuatia uamuzi wake wakati huo wa kulipiga marufuku shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.
Kesi hiyo inaendelea wakati Shirika la Msalaba Mwekundu limetahadharisha leo Ijumaa kuwa mfumo wa misaada ya kibinadamu huko Gaza unakaribia kuporomoka kabisa ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa ili kurejesha mtiririko na usambazaji wa misaada ya kibinaadamu kwa Wapalestina wapatao milioni 2.4.
Tangu Israel ilipochukua hatua ya kuzuia misaada, Umoja wa Mataifa umekuwa ukitahadharisha juu ya hali mbaya ya kibinaadamu ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa viwango vikubwa vya njaa.
Soma pia: Marekani yaitetea Israel kuzuia misaada kuingia ukanda wa Gaza
Naibu Mkurugenzi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC, Pascal Hundt amesema wananchi wa Gaza wanakabiliwa na madhila ya kila siku huku wakihatarisha maisha yao kutokana na mapigano, wanahamishwa kila kukicha wanakabiliana na matokeo ya kuzuiliwa misaada ya dharura ya kibinadamu, akisisitiza kuwa hali hiyo haipaswi na haitakiwi kuendelea.
Mapigano na juhudi za amani katika mzozo wa Gaza
Juhudi za kusitisha mapigano huko Gaza bado zimekwama huku Israel ikiwa imezuia kuanzia Machi 2 mwaka huu, uingizwaji wa chakula, mafuta, dawa na misaada mingine ya kibinadamu katika eneo hilo lililokumbwa na vita.
Mashambulizi pia yanaendelea huku Israel ikichukua udhibiti wa sehemu kubwa za ardhi ya Palestina , kwa madai kuwa ni hatua za kuishinikiza Hamas kuwaachilia mateka zaidi ambao bado wako mikononi mwao. Israel ilishambulia usiku wa jana kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bureij na kusababisha maafa kama anavyoelezea Mohammed Abu Zeina aliyewapoteza ndugu zake:
" Baba, watoto na wajukuu, mke, dada yangu, na majirani kadhaa wameuawa kama mashahidi. Kufikia sasa, kuna karibu watu tisa waliouawa."
Soma pia: Netanyahu akosoa uamuzi wa ICJ ni 'uamuzi wa uwongo
Hayo yakiarifiwa, kundi la wanaharakati wanaoandaa mashua ya kusafirisha misaada kuelekea Gaza wamesema meli yao ilishambuliwa na droni za Israel usiku wa kuamkia leo katika bahari iliyo chini ya sheria za kimataifa karibu na Malta walipokuwa wakielekea katika ardhi ya Palestina. Serikali ya Malta imeeleza kuwa watu wote 16 waliokuwamo katika meli hiyo wako salama.
(Vyanzo: Mashirika)