ICC yawasweka jela maafisa 2 Jamhuri ya Afrika ya Kati
25 Julai 2025Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imemhukumu afisa mmoja mwandamizi wa zamani wa kandanda katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na mwanamgambo mmoja aliyejulikana kwa jina la utani kama "Rambo" kwa uhalifu wa kivita walioufanya wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka 2013 na 2014.
Waziri wa zamani wa michezo Patrice Edouard Ngaissona alikuwa kiongozi mkuu wa wanamgambo wa Kikristo wakati nchi hiyo ilipotumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, naye Alfred Yekatom ambaye ni mbunge wa zamani, alikuwa kama kamanda wa wanamgambo hao.
Mahakama hiyo ya ICC imemhukumu Yekatom miaka 15 jela kwa vitendo 20 vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji na mateso.
Ngaissona naye amepewa kifungo cha miaka 12 jela kutokana na kupatikana na hatia ya visa 28 vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.