Mahakama ya Afrika ya Haki kusikiliza kesi ya DRC vs Rwanda
26 Juni 2025Mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu iliyopo Arusha Tanzania imesema kwamba inayo mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri lililofunguliwa na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ikiituhumu Rwanda kuunga mkono kundi la waasi la M23, linalosababisha machafuko Mashariki mwa Kongo. Awali Rwanda ilipinga shauri hilo kwa kudai kuwa mahakama hiyo ya haki za binadamu haina mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo.
Jaji Rafaa Ben Achour wa Mahakama hiyo wakati akisoma maamuzi hayo ya mahakama amesema kuwa pamoja na maamuzi hayo, mahakama imetoa siku 90 kwa Rwanda kujibu hoja za Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, na siku 45 kwa Kongo kuzipitia na kuzifanyia tathimini hoja za Rwanda kabla Mahakama hiyo haijakutana tena kusikiliza shauri hilo na kutoa maamuzi.
Alisema "Mahakama hii ina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dhidi ya Rwanda, hata hivyo Mahakama inapaswa kuzingatia iwapo katika mazingira fulani inaweza kutumia mamlaka yake ya kieneo pale ambapo ukiukwaji unaodaiwa ulitokea nje ya mipaka ya nchi inayoshitakiwa.”
Kongo inashutumu Rwanda kwa kukiuka haki za binaadamu
Kongo inaituhumu Rwanda kwa kukiuka haki za binadamu, ikiwamo mauaji, ubakaji, uharibifu wa mali pamoja na kuwafanya zaidi ya watu laki tano kuyakimbia makazi yao huku karibu watoto 20,000 elfu ishirini wakikosa huduma za msingi ikiwamo elimu.
Katika kesi hiyo DRC imeiomba mahakama iiamuru Rwanda kuondoa vikosi vyake nchini humo, kusitisha msaada kwa kundi la M23, pamoja na kutoa fidia kwa madhara yaliyosababishwa. DRC inasema maamuzi ya leo yanatoa mwanga kwa nchi hiyo.
"Ni maamuzi yanayotoa mwanga katika kupigania haki za binadamu mashariki mwa Kongo pamoja na malalamiko kati ya nchi wanachama kuhusu kesi za haki za binadamu barani Afrika,” alisema Samuel Mbemba, Waziri wa Sheria wa Kongo
Hata hivyo Rwanda imekuwa ikikanusha vikali madai hayo yanayotolewa na DRC.