SiasaUturuki
Mahakama ya Uturuki yaamuru kuzuiliwa kwa Meya wa Istanbul
23 Machi 2025Matangazo
Mahakama ya Uturuki imeamuru Jumapili kuwekwa kizuizini Meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu, mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan kabla ya kuanza kusikilizwa kesi inayomkabili.
Imamoglu alikamatwa siku ya Jumatano, ikiwa ni siku kadhaa kabla mkutano wa chama kikuu cha upinzani cha CHP, ambao anatarajiwa kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Uturuki.
Kukamatwa kwake kumesababisha maandamano ya kila usiku nchini kote, hadi watu 300,000 walikusanyika Istanbul siku ya Ijumaa usiku pekee kulingana na takwimu za chama chake cha CHP.
Meya huyo maarufu anakabiliwa na shutuma za ugaidi na ufisadi katika kesi mbili tofauti. Amri ya hakimu ya leo Jumapili ya kuzuiliwa kabla ya kesi inahusiana na tuhuma za rushwa.