Mahakama Japan yaamuru kuvunjwa kwa Kanisa la Unification
26 Machi 2025Mahakama nchini Japan imefuta hadhi rasmi ya Kanisa la Unification, hatua itakayolazimisha kanisa hilo kulipa kodi na kuuza mali zake. Uamuzi huo umetokana na uchunguzi uliofuatia kuuawa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, mwaka 2022, ambapo muuaji alidai kuchukizwa na uhusiano wa karibu kati ya Abe na kanisa hilo.
Serikali ya Japan iliiomba mahakama kulifuta kanisa hilo kutokana na mbinu zake za kukusanya fedha ambazo zilikuwa zikiumiza familia za wafuasi wake. Kanisa hilo lenye makao yake Korea Kusini limepinga vikali uamuzi huo likidai kuwa ni ukiukwaji wa uhuru wa dini na haki za binadamu.
Soma pia:Japan yamuaga Shinzo Abe
Kanisa hilo, maarufu kama "Moonies," lilikuwa na uhusiano wa karibu na wanasiasa wengi wahafidhina wa Japan tangu liliposajiliwa rasmi mwaka 1968. Huu ni uamuzi wa kwanza wa aina hii dhidi ya kundi la kidini nchini humo.