Magenge yenye silaha yateka nyara zaidi ya watu 50 Nigeria
3 Agosti 2025Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti binafsi ya ufutiliaji wa migogoro iliyoandaliwa kwa ajili ya Umoja wa Mataifa na kuonekana na shirika la habari la AFP leo Jumapili.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba watu wenye silaha walishambulia kijiji cha Sabon Garin Damri katika jimbo la Zamfara siku ya Ijumaa, ikiwa ni shambulio la hivi karibuni katika eneo ambalo watu wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu kutokana na kuhangaishwa na magenge ya wahalifu wanaoteka nyara watu kwa ajili ya kulipwa fidia, kupora vijiji na kuwatoza kodi.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa tukio hilo ndio la kwanza la "utekaji mkubwa wa watu" katika eneo la Bakura lililopo katika jimbo la Zamfara na kwamba mwelekeo huo wa utekaji nyara unatia wasiwasi.
Msemaji wa polisi katika mkoa wa Zamfara hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu tukio hilo.
Mgogoro wa uhalifu wa magenge nchini Nigeria ulianza kama mzozo wa ardhi na kupigania haki za maji kati ya wafugaji na wakulima, lakini sasa umegeuka na kuwa uhalifu uliopangwa, ambapo magenge huwalenga watu vijijini ambao mara nyingi hawapati msaada wowote kutoka kwa serikali.