Magenge ya wahalifu yaua maafisa 13 wa usalama Nigeria
10 Agosti 2025Magenge haya, yamekuwa yakitesa jamii za kanda ya kaskazini-magharibi na kati mwa Nigeria kwa miaka mingi—wakivamia vijiji, kuwateka nyara wakaazi, na kuchoma nyumba baada ya kuzipora.
Hamisu Faru, mbunge wa eneo hilo amesema majambazi hao walivamia kijiji cha Adabka kilichopo wilayani Bukkuyum usiku wa Ijumaa na kuwateka baadhi ya wakazi, walitega mtego na kuwashambulia kwa risasi polisi na walinzi wa kujitolea waliokuwa wakiwafuatilia ili kuwaokoa mateka.
Licha ya kupelekwa kwa vikosi vya kupambana na magenge ya wahalifu tangu mwaka 2015, na kuundwa kwa kikosi cha wanamgambo na serikali ya jimbo la Zamfara miaka miwili iliyopita, ghasia bado zinaendelea. Serikali ya shirikisho na ya jimbo zimekuwa zikitia saini mikataba ya amani na magenge hayo kwa miaka mingi, lakini makubaliano yameshindwa kudumu.