Magazeti ya Ujerumani ya Leo
31 Machi 2004Kwanza tuanze na gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Düsseldorf, limeandika hivi:
+ Kwa miezi sasa yalidumu mabishano baina ya mawaziri Wolfgang Clement na Jürgen Trittin juu ya suala la moshi unaotoka viwandani, na mwishowe baada ya makelele mengi kumepatikana suluhisho ambalo halisaidia kuwa na hewa ilio safi. Kwamba Ujerumani katika siku za mbele itapunguza kutoa moshi wa viwandani wa kiasi cha tani milioni mbili ni jambo ambalo halitabadilisha sana uchafuzi wa hewa, na pia ni jambo ambalo halitapunguza hali ya mivutano ndani ya serekali ya mseto.+
Gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG liliandika:
+ Namna waziri wa mazingira na makamo wa Kansela walivoregeza kamba katika yale mazungumzo ya usiku baina ya wakuu wa vyama vya serekali ya mseto ni jambo lililomvunja moyo kila mtu ambaye alikipigia kura Chama cha Kijani kutokana na msimamo wake wa kupigania usafi wa mazingira. Angalau sasa wapigaji kura wameweza kutafautisha baina ya mbivu na mbichi; ni kama hivi: kwa wale wanaopigania kikweli kwamba usafi wa mazingira ufanyike kwa mitindo ya kisasa na mara nyingi wakiwa wabishi na wenye misimamo mikakamavu hata kusababisha mapambano ndani ya Chama chao cha Kijani, duru hii ya mazungumzo, katika ngazi ya kiserekali, imewapa ushindi wale watu waliokuwa tayari kujirekebisha ili kuhifadhi nyadhifa zao. Ni Kansela ndiye anayebeba dhamana ya kushindwa huku kwa siasa ya mazingira.+
Gazeti la HEIBRONNER STIMME liliandika hivi:
+ Mabishano kuhusu maelezo juu ya viwango vya juu kabisa vya moshi vinavoruhusiwa kutolewa na viwanda yanadhihirisha mengi kuhusu uzito ilionao kila upande ndani ya serekali ya mseto ya Ujerumani. Kwa Kansela Schroader Chama cha Kijani cha mazingira, kama kilivokuwa Chama cha Free Democratic, FDP, wakati wa Kansela Helmut Kohl, ni chama cha kumpatia yeye wingi wa kihesabu bungeni, licha ya matatizo yanayomuudhi yanayosababishwa na chama hicho. Na hata kwa masuala ya zamani yanayoshughulikiwa na viongozi wa Chama cha Kijani kuna kipimo. Kwa hivyo waziri wa uchumi, Wolfgang Clement, asiadhibiwe ikiwa atalitupilia tena mbali suluhisho hili lililofikiwa kwa jitihada ya muda mrefu. Viongozi wa Chama cha Kijani wamekuwa watu wasiojitakia makuu kwa yale wanayoyalengea, wametosheka kuwa zizi la vijana.+
Gazeti la BERLINER ZEITUNG, kuhusu mada hiyo hiyo, lilikuwa na haya:
+Jee kumepatikana suluhu katika mabishano kuhusu kiwango cha moshi kinachotolewa na viwanda? Kwa hakika hakuna kilichopatikana. Trittin na na Chama cha Kijani hawasaidiwi kwa kujipa moyo. Wameshindwa vibaya. Hamna mtu anayetaka kufungamanishwa masuala ya uchumi na mazingira kutokana na ongezeko la watu wasiokuwa na kazi hapa Ujerumani.+
SÜDDEUTCHE ZEITUNG linalochapishwa Munich liliandika kama hivi:
+Kwa bahati mbaya huu mfumo wa viwango vya moshi unaotoka viwandani umewekwa nyuma kabisa katika umuhimu kutokana na haya mabishano yaliozuka baina ya waziri wa uchumi, Wolfgang Clement, na waziri wa mazingira, Jürgen Trittin. Kwa muda kumechipuka hisia kwa wale walio na maslaha kwamba waziri Trittin ameuwasilisha mpango wa kishetani ili kuutia kwenye dhiki uchumi wa Ujerumani. Lakini lengo la waziri huyo ni kutekeleza mwongozo wa Jumuiya ya Ulaya ambayo tume yake imejaribu, kwa mara ya kwanza, kukabiliana na mtindo wa kuraruana katika mashindano ya kibiashara baina ya nchi wanachama.+
Gazeti linalochapishwa Düsseldorf la HANDELSBLATT linaamini kama hivi:
+ Viwanda vya Ujerumani vinaweza kuishi na suluhu hiyo iliofikiwa baina ya waziri wa uchumi, Wolfgang Clement, na mshindani wake, waziri wa mazingira, Jürgen Trittin. Mchanganyiko wa nishati tafauti ambao unaweza kutumiwa hapa Ujerumani kwa njia ya kuvipatia viwanda faida katika mashindabno ya kibiashara uko mbali kufikiwa. Waziri Clement yuko mbali kuweza kuwasilisha mpango wa nishati utakaoihakikishia Ujerumani kuwa mahala pazuri pa kuwekeza viwanda. Waziri huyo wa Chama cha Social Democratic, hata hivyo, anaona mbali kuweza kuyatengeneza yale yalioharibika katika malumbano haya yaliotokea. Mipango ya waziri Trittin ya kuyasafisha mazingira yanauumiza uchumi wa Ujerumani kwa karibu ya Euro bilioni 20 kwa mwaka.+
Mwishowe tulitupie jicho gazeti la FREIE PRESSE la mjini Chemnitz:
+ Waziri Trittin ingefaa angetambua zamani kwamba alikuwa hana nafasi hata kidogo kufaulu katika malumbano hayo. Katika mzozo huu ulioriopuka tena baina ya mazingira na uchumi, Wolfgang Clement ameungwa mkono zaidi. Mara hii lilikuwa sio suala la malumbano makali baina ya wale wanaoshabikia uchumi upanuke kwa njia yeyote na wale walio washabiki wa mazingira kuwa masafi. Lakini mara hii waziri Clement aliungwa pia na vyama vya wafanya kazi na mawaziri wakuu wa serekali za mikoa. Wote hao walikuwa na wasiwasi uliokuwa wa haki. Wasi wasi huo ni kwamba kila mbinyo ukizidi kwa viwanda vilinde zaidi mazingira ndipo wanabiashara zaidi wanapoamuwa kupeleka viwanda vyao nje ya nchi, hivyo kusababisha ukosefu wa kazi zaidi hapa Ujerumani.+
Basi hayo ni kwa leo kutoka magazetini.