Magazeti ya Ujerumani wiki hii yamejishughulisha na matokeo mbali mbali barani Afrika
3 Oktoba 2003
Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari wiki hii ni uchaguzi wa Rwanda;Kongo yaafikiana mapatano ya ushirikiano na nchi jirani;Vikosi vya kuhifadhi amani vya UM vyachukua jukumu lao nchini Liberia,Kanzela Schröder kufungua Chuo Kikuu cha kijerumani mjini Cairo na kinyan'ganyiro kati ya Libya,Afrika Kusini na Misri kuania tiketi ya kwanza kabisa ya kuandaa kombe la Dunia la kabumbu barani Afrika.
Gazeti la TAGESZEITUNG linalochapishwa mjini Berlin chini ya kichwa cha habari: RWANDA YACHAGUA NA MATOKEO YAKIJULIKANA TANGU MWANZO,lachambua: "Ili kunyakua viti Bungeni katika uchaguzi wa kwanza huru,wameania viti wafuasi pekee wa Rais Kagame."
Gazeti likaendelea kuandika nchini Rwanda,uchaguzi wa kwanza huru tangu nchi hii kujipatia uhuru 1962.Upigaji kura huo wakati huo huo unakamilisha kipindi cha mpito cha Ruanda kuelekea demokrasia-utaratibu ambao ulianzia na kura ya maoni juu ya katiba hapo Mei na uchaguzi wa rais hapo August mwaka huu. Hakujatarajiwa matokeo ya kusangaza mno sawana ilivyokua katika kura ya maoni iliotangulia ambamo warwanda takriban kwa kauli moja waliitikia mwito wa serikali. TAGESZEITUNG likaongeza, " Vyama vyote vya kisiasa vilivyigombea uchaguzi vilimuungamkono Rais kagame katika uchaguzi wa urais wa August.25 ambae alijipatia 95% ya kura.Katika uchaguzi ule,mpinzani mkuu wa Kagame Faustin Twagiramungu alibidi kuogombea uchaguzi huo kama mtetezi wa kujitegemea binafsi kwavile chama chake cha MDR kilipigwa marufuku kushiriki kwa tuhuma za kupalilia hamasa za kikabila." TAGESZEITUNG mwishoe linakumbusha kwamba, rais wa mwisho kutoka chama cha MDR Celestin Kabanda katika uchaguzi huu alinyimwa hata haki ya kugombea.Yeye kama vile mpinzasni mwengine Jean-Baptiste Sindikubwabo wametuhumiwa eti walifanya udanganyifu katika utiaji saini zao.Hii ni kwa muujibu wa tume ya Uchaguzi ilivyoamua ijumaa iliopita.Chama kipya kilichofuatia kile cha MDR hakikuruhusiwa kushiriki. Gazeti lamaliza:
"Bunge jipya la rwanda kwahivyo, halitakua jukwaa la malumbano ya kisiasa n a kutoka wabunge 80 wa bunge hilo ni 53 tu waliochaguliwa moja kwa moja na wapigakura." Tukiuupa kisogo kwa sasa uchaguzi wa Rwanda tugeukie nchi jirani ya Kongo: Chini ya kichwa cha habari: KONGO YAAFIKIANA MKATABA NA NCHI JIRANI, gazeti linalochapishwa mjini Munich-SÜDDEUTSCHE ZEITUNG laandika:
"Baada ya vita vya miaka kadhaa,waakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo na wa nchi jirani wameafikiana mkataba wa ushirikiano.Ni mkataba wa kuchangia utaratibu wa kurejesha amani katika Afrika ya Kati-hii ni kwa muujibu ilivyoarifiwa kandoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Um mjini New York.Huko Rais wa Kongo na wa Burundi pamoja na waziri-mkuu wa rwanda na mawaziri wa nje wa Angola na Uganda,walikutana kwa kikao cha masaa 2. Msemaji wa UM Fred Eckhard alisema viongozi hao wameafikiana mapatano ya ushirikiano na ujirani mwema.Nchi hizi 5 zilihusika moja kwa moja na vita vya Kongo-vita ambavyo vimehilikisha mamilioni ya watu." SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lakumbusha mwishoe, kwamba katika mkutano huo,walihudhuria pia waakilishi wa Msumbiji,Tanzania na Afrika Kusini-nchi zilizochukua juhudi za upatanishi.
Kutoka mzozo wa Kongo na enzi mpya ya ujirani mwema inayotarajiwa, tugeukie Afrika magharibi na balaa la Liberia: Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU chini ya kichwa cha habari: "VIKOSI VYA KUHIFADHI AMANI VYA UM VYACHUKUA JUKUMU LAO NCHINI LIBERIA" laandika: "Kuanzi jumatano UM ukijaribu kusimamia usalama nchini Liberia.UM umechukua dhamana ya usalama kutoka mikono ya kikosi cha Afrika magharibi Ecomil ambacho askari wake 3.500 wanashika zamu kwa niaba ya UM."
FRANKFURTER RUNDSCHAU lakumbusha: "Baraza la Uslama la UM limeidhinisha kupelekwa Liberia hadi askari 15.000 wa kuhifadhi amani na kikosi cha polisi cha askari 1115.Kwa kiwango kikubwa kama hicho,UM ulihifadhi amani katika nchi jirani ya Sierra Leone na kuwapokonya wapiganaji silaha. Tayari sasa,vikosi vya UM vinavyochangiwa na Nigeria,Guinea-Bissau,Senegal,Mali na Ghana vinashika zamu katika sehemu mbali mbali za mji mkuu Monrovia,Buchanan,Kakata na Totoa.Asakri hawa wanawapa raia hisia ya usalama."
Kutoka mzozo wa Liberia,gazeti la TAGESZEITUNG mjini Berlin, laitupia macho ziara inayoanza mwishoni mwa wiki hii ya kanzela Gerhard Schröder wa Ujerumani nchini Misri n a eneo la Ghuba: Chini ya kicha cha habari:"CHUO KIKUU CHA UJERUMANI KWA MISRI"- Tageszeitung laandika kuwa,Kanzela Schröder atafungua jumapili hii mjini Cairo Chuo Kikuu cha kwanza kabisa cha nchi ya kigeni.Katika Chuo hicho cha kibinafsi,wanatazamiwa wanafunzi 4.800 kujifunza. Gazeti laandika:
"Hii itakua hatua ya mwanzo ya mfumo wa elimu ya Ujerumani. Jumapili hii, Kanzela Schröder akifuatana na mwenyeji wake Rais Hosni Mubarak,watazindua Chuo Kikuu cha kwanza kabisa cha kijerumani nchi za n'gambo.Chuo hiki kitachukua katika awamu yake ya kwanza jumla ya wanafunzi 700. Mwishoe lakini, chuo hiki kitakua na hadi wanafunzi 4.800 ambao watajifunza fani kama vile za ufundi wa komputa na wa mawasiliano ya habari,madawa na kadhalika."
Tumalize ukaguzi huu wa AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI kwa kudondoa kutoka gazeti la jiji la Düsseldorf la RHEINISCHE POST ambalo limenatupa mwangaza juu ya kinyan'ganyiro kinachoendelea barani Afrika cha kuania tikiti ya kuandaa Kombe la kwanza la kabumbu la dunia barani afrika 2010. LIBYA YAVUTIA SANA KATIKA KUJITEMBEZA KWAKE WIKI HII-laandika Rheinischepost.Libya haikubakisha kitu huko Zurich,Afrika Kusini yajitembeza kwa zana na viwanja vyake maridadi ilivyo navyo tayari pamoja na maarifa ilionayo katika kuandaa mashindano makubwa .Libya,Tunisia,Misri na Morocco pamoja na Afrika kusini zaania kuanda Kombe la dunia.
Rais wa FIFA Sepp Blatter amenukuliwa kusema, wiki hii wakati wa tarehe ya mwisho ya kutoa hati za kugombea huko Zurich,kila mmoja ameonesha hamu kubwas na nguvu zake za kuandaa dimba. Blatter aliovutiwa zaidi na Libya,kwani imaehidi kutumia hadi dala bilioni 3.6 kwa maandalio ya kombe la dunia,kujenga viwanja 8,barabara na mawasiliano pamoja na mahoteli. Wakati Afrika kusini imejitoa uwanjani na viwanja vyake 13 katika miji yake 11 mbali mbali,ambavyo vitapanuliwa na kufanywa vya kisasa kwa kima cha dala milioni 350,wagombeaji wote waliosalia walijitoa kwa viwanja 8 kila nchi moja.
Gazeti linakumbusha kwamba, Afrika kusini ambayo inaungwamkono na wafadhili kama kampuni la coca Cola,la magari la BMW na PHILIPS,linagombea kwa mara ya pili kuandaa kombe la dunia.Moroko inagombea kwa mara ya 4. Miaka 2 nyuma FIFA iliamua 2010 itakua zamu ya bara la Afrika kuandaa kombe la dunia. Uamuzi nchi gani itaanda Kombe hilo lwa kwanza la dunia barani Afrika,utakatwa mjini Paris Mei 20,hapo mwakani.