Magazeti ya Ujerumani hii leo
6 Aprili 2004Kutoka gazeti la OFFENBURGER TAGEBLATT tunaseoma kama hivi:
+ Hali ya mambo katika Iraq itazidi kuwa mbaya kwa Marekani. Kwa vile kuna uchaguzi wa urais wa Marekani hapo Novemba mwaka huu, mtu lazima atilie maanani kwamba utayarifu wa watu kutumia nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati utaengenezeka. Wa-Iraqi wanataka Rais Bush asichaguliwe tena kuwa rais wa Marekani, na huenda wanahisi rais mpya wa Marekani atayaondosha majeshi ya nchi yake kutoka Iraq. Ndio maana Wa-Iraqi wanataka kuitayarisha nchi yao iwe Vietnam ya pili kwa Wamarekani. Umma na raia wa Kimarekani wanahofia zaidi nchi yao kushindwa huko Iraq kama vile ilivotokea Vietnam hapo kabla. Katika Vietnam Marekani ilipata pigo la mwanzo na la pekee ambalo hadi sasa athari zake zingaliko.+
Gazeti la MANNHEIMER MORGEN lilikuwa na haya ya kusema:
Huko Marekani na duniani kote sasa inatambuliwa kwamba dola pekee duniani, yaani Marekani, haiwezi peke yake kumudu kuleta utulivu katika Iraq. Wamarekani wanahitaji msaada, lakini msaada wa aina gani ni jambo ambalo bado sio wazi. Kutokana na hatari za kiusalama, hamna nchi inayoshikilia kupeleka majeshi yake kwa shughuli za kuweka amani chini ya kibali cha Umoja wa Mataifa. Wakiwa hawana la kufanya, Wamarekani kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa wakiwapa Wa-Iraqi dhamana zaidi za kuiendesha nchi yao. Hata hivyo, katika siku chache zilizopita imedhihirika kwamba majeshi yao hayana uwezo wa kuleta utulivu katika nchi hiyo.+
Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG kutoka Frankfurt an der Oder lilifikiria namna hivi:
+Tangu sasa umeshindwa ule mpango wa kuupandikiza mfumo wa Ki-Magharibi nchini Iraq. Kwa mujibu wa fikra za makamo wa Rais wa Marekani, Dick Cheney, makamo wa wazziri wa ulinzi, Wolfowitz, na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa, Bibi Condoleze Rice, ni kwamba kungepatika kama ile athari ya nyumba ya karata, yaani karata moja ikianguka basi karata nyingine zinafuata kuanguka. Kwanza imeanguka Iraq, halafu itafuata kuporomoka Iran, mwishowe Syria itafuata na huenda baadae Saudi Arabaia; hivyo kulifanya eneo lote la Mashariki ya Kati liambatane na mfumo uliofikiriwa na Marekani. Lakini makisio hayo yalikuwa ya makosa kwa vile hayajitilia maanani mazingira ya kisiasa, kiuchumi, kidini na kitamaduni ya Iraq.+
FRANKFURTER RUNDSCHAU nalo lilikuwa na haya ya kusema:
+ Ghasia na vurugu za kuchukiza zilizotokea katika mji wa Falludja zinatoa ishara ilio wazi zaidi ambayo inafikia kote nchini Iraq. Kuraruliwa maiti za wafanya kazi wanne wa kampuni ya usalama ya Marekani ambao walikuwa wanaendesha shughuli za kijeshi kumeangaliwa na baadhi ya magazeti ya kimkoa kuwa ni kulipiza kisasi kwa kitendo cha Israel cha kumuuwa mkuu wa Chama cha Hamas cha Wapalastina, Sheikh Yassin. Pale mizozo ya huko Palastina na Iraq inapochanganyika, basi lile lengo la Rais Bush la kuivamia Iraq ambalo alikuwa halitaki litakuwa limefikiwa: nalo ni kuweko vurugu katika Iraq nzima na karibuni kuweko uasi katika eneo zima la Mashariki ya Kati.+
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lilijishughulisha na kashfa ya Ernest Welteke, Rais wa Benki Kuu ya Ujerumani. Liliandika hivi:
+ Kashfa hiyo, kwa haki, inazusha hisia fulani. Ernst Welteke, rais wa Benki Kuu ya Ujerumani, pamoja na sehemu ya familia yake walibidi walipie gharama za kukaa kwao katika Hoteli ya Adlon ya mjini Berlin mwishoni mwa mwaka 2,001. Kukaa kwao kwa siku nne kuligharimu Euro 7661. Gharama hiyo ilibebwa na Dresner Bank kwa vile benki hiyo iliandaa sherehe ya kuanzishwa sarafu ya EURO, naye Bwana Welteke alitaka kutokeza katika sherehe hiyo pembeni mwa waziri wa fedha, Hans Eichel, kama mtu muhimu. Bwana Welteke hajaalikwa katika sherehe hiyo kwa vile yeye ni mtu mzuri, lakini kwa vile yeye ni Rais wa Benki Kuu ya Ujerumani. Ikiwa mtu ataiangalia sherehe hiyo ya kujitangaza Dresner Bank kuwa ni shughuli ya kikazi, basi Benki Kuu ya Ujerumani ingebidi kulipia gharama za mkuu wake kwa kuweko huko Berlin, kwa vile Bwana Welteke ni mfanya kazi wa serekali. Pia ikiwa Benki Kuu ya Ujerumani, kutokana na majukumu yake, inatakiwa na serekali kuwa ni taasisi inayojitegemea na huru, wakuu wanane wa jopo lake la uongozi, wanne wakiwa wanateuliwa na serekali ya Ujerumani na baraza la serekali za Mikoa, kisheria na kiadilifu wanahitajika waambatane na sheria zile zile k zinazowahusu wafanya kazi wa serekali.
Mwishowe gazeti la BONNER GENERAL ANZEIGER liliandika hivi:
+ Sasa mambo yamechelewa sana. Sifa nzuri ya Rais wa Benki Kuu ya Ujerumani imeharibika. Matokeo yake yatakuwa sio tu kuchunguza kama atachukuliwa hatua kufuatana na sheria za wafanya kazi wa serekali. Yeye mwenyewe Welteke binafsi atafikiria kama anaweza kubakia katika wadhifa huo wa kuutumikia umma, umma ambao unataka mwenye kuukamata wadhifa huo awe msafi kabisa katika masuala yanayohusiana na fedha.+
Miraji Othman