Magazeti ya Ujerumani hii leo
15 Julai 2004Gazeti la DIE WELT limeutathmini namna hivi uamuzi wa Rais Chirac:
+ Uamuzi huo unaingia akilini, kwani mwishowe katiba ya Jumuiya ya Ulaya ndio itakayoamuwa juu ya maisha ya kila siku ya Wafaransa. Ufaransa sasa ni miongoni mwa nchi ambazo wananchi wao watapewa haki pia kuamuwa juu ya katiba hiyo. Mseto wa vyama vyote vya kisiasa hapa Ujerumani unahofia kuchukuwa hatua kama hiyo. Hapo baadae, kama ilivokuwa kabla, hapa Ujerumani Jumuiya ya Ulaya itafahamika kama ni mradi wa watu wa tabaka ya juu, watu wenye kujuwa mambo, huku watu wa kawaida wakiwa hawaufahamu mradi huo. Ikiwezekana watu hao hawataingizwa katika mradi huo. Lakini katika kuwauliza wananchi kuna nafasi ya mamlaka ya mradi huo wa katiba kueleweka zaidi na kuuamsha uzalendo wa Ki-Ulaya, mambo ambayo yanakosekana hivi sasa.+
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika hivi:
+ Uamuzi huo sio wa kimapinduzi katika nchi ilioundwa kama vile Ufaransa. Lakini uamuzi huo ni wa ujasiri kwa rais ambaye serekali yake iko katika mkwamo mkubwa- nao ni kutaka kufanya mabadiliko makubwa ambayo yatawatia moyo wananchi. Mabadiliko hayo yanawatia wasiwasi Wafaransa kama vile yanavowatia wasiwasi Wajerumani juu mipango ya serekali ya Kansela Schroader katika kupunguza matumizi ya huduma za kijamii nchini mwake. Rais Chirac anachukuwa hatua ya hatari katika jambo moja, nalo ni kwamba pale Wafaransa, ikiwezekana, katika kura hiyo ya maoni wakaelezea zaidi maoni yao kuhusu serekali ya waziri mkuu Raffarin kuliko juu ya katiba yenyewe ya Ulaya.+
Kwa ufupi, gazeti la FINANCIAL TIMES la hapa Ujerumani liliandika hivi:
+ Jacques Chirac yuko katika hatari, nayo ni kwamba mwenendo wa kuiunganisha Ulaya unaweza ukashindwa. Kura ya Wafaransa itakayosema hawaitaki katiba ya Jumuiya ya Ulaya itakuwa na uzito mkubwa zaidi kuliko kura ya Waengereza itakayoikataa katiba hiyo, jambo ambalo linatarajiwa. Ikiwa Wafaransa wataipinga hati ya katiba hiyo, na Waengereza nao wakaikataa, basi tena ile fikra nyingine itakuwa wazi, nayo ni kuwa na Jumuiya ya Ulaya yenye nchi fulani asisi, ambapo Ujerumani na Ufaransa ndizo zitakuwa injini.+
Tubadilishe maudhui.
Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG limeitupia jicho ile ripoti ya tume ya uchunguzi huko Uengereza ambayo haijamuona waziri mkuu wa nchi hiyo, Tony Blair, kuwa alilidanganya kwa makusudi taifa lake katika kupata habari za kijasusi kabla ya kuingia katika vita vya Iraq. Liliandika hivi:
+ Tony Blair asingekuwa Tony Blair ingekuwa hajatumia yale maneno ambayo yalidai kwamba Iraq ilimiliki silaha za maangamizi na baadae kusema kwamba matamshi hayo yalikuwa ni kitendo kikubwa cha kihistoria. Alipokutana na waziri mkuu wa Italy, Berlusconi, Tony Blair alisema kwamba hivi sasa dunia imekuwa yenye usalama zaidi bila ya Saadam Hussein. Hapa ukweli unaepukwa kuangaliwa machoni, mtu akiitambuwa hali mbaya ya usalama ilivyo sasa huko Iraq na hatari ya hali hiyo kusamabaa katika eneo hilo zima la dunia. Ukweli ni zaidi ya huo, nao ni kwamba dunia imeondokana na dikteta huyo, lakini sasa yanatamba huko Iraq makundi mbali ya kigaidi. Ukweli ni pia kwamba kushughulikia zaidi kuwa na mabadiliko ya serekali huko Iraq kulichukuwa umuhimu zaidi kuliko suala la kupambana na kusamabaa silaha za maangamizi.+
Pia, tena tubadilishe mada.
Waziri wa familia wa Ujerumani, Bibi Scmidt, kupitia sheria, atahakikisha kwamba hapa Ujerumani kunajengwa shule zaidi za chekechea. Kwa mujibu wa gazeti la WETZLARER NEUEN ZEITUNG:
+ Mswaada huo wa waziri Schmidt ni zaidi kuwa ni hatua ya kwanza. Chama cha Kijani kinalaumu kwa haki kukosekana sheria ambapo mtu anaweza kudai kuwa na haki hiyo ya kupatiwa nafasi katika shule ya chekechea kwa ajili ya mwanawe. Mzazi anayelea peke yake mtoto mdogo au wazazi ambao wote wawili wanafanya kazi hutegemea tu nia njema ya serekali za mitaa.+
Gazeti la MANNHEIMER MORGEN liliiona hatua hiyo kuwa ni nzuri na liliandika hivi:
+ Sheria hiyo haitoifanya Ujerumani iwe ni pepo kwa familia. Lakini sheria hiyo, kwa mara ya kwanza, itakuwa zaidi ya kupiga domo tu wapiganiaji wa kampeni za uchaguzi, kama ilivokuwa katika miaka iliopita. Kwamba hatua hiyo kubwa haijaweza kuchukuliwa hadi sasa, sio kosa la serekali. Mazingira yenye kupendelea familia yanaweza kusaidiwa kisiasa, lakini yanahitaji msaada wa jamii nzima. Jambo hilo linaonekana linatambuliwa, japokuwa tu polepole.+
Miraji Othman