Maelfu hatarini kufa kwa njaa mji uliozingirwa wa El-Fasher
5 Agosti 2025Tangu Mei 2023, mji wa El-Fasher umekuwa ukizingirwa na wapiganaji wa RSF walioko vitani dhidi ya jeshi la taifa. Njia kuu zote zimefungwa, hali inayozuia misaada ya kibinadamu kuwafikia wakazi waliokwama. Sudan imeendelea kuituhumu UAE kwa madai ya kuisaidia RSF, ikiwemo kutuma mamluki kutoka Colombia kupigana bega kwa bega na kundi hilo.
Kwa mujibu wa shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, bei za bidhaa muhimu kama mtama na ngano zimepanda kwa zaidi ya asilimia 400, huku vituo vya afya na masoko vikilengwa na mashambulizi ya RSF.
Familia nyingi zimebaki kula majani ya mifugo na mabaki ya vyakula, huku majiko ya kijamii yakifungwa kutokana na uhaba wa misaada. Hali hiyo imezidishwa na mvua za masika ambazo zimeharibu miundombinu na kufanya maeneo mengi kufungwa kabisa.
Watoto ndio wanaoathirika zaidi
Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, karibu asilimia 40 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano mjini El-Fasher wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na asilimia 11 wakiwa katika hali ya hatari ya kiafya.
Hali hiyo imeelezwa ma mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, Sheldon Yett, kuwa ni tishio la kizazi kizima kupotea kutokana na ukosefu wa msaada wa haraka.
"Watoto wanakufa kwa njaa, magonjwa, na vurugu. Wamekatishiwa huduma za msingi zinazoweza kuokoa maisha yao. Tuko kwenye ukingo wa madhara yasiyorekebishika kwa kizazi kizima, si kwa sababu hatuna uwezo, bali kwa sababu tunashindwa kuchukua hatua kwa haraka inavyohitajika," alisema Yett.
Kwa ujumla, hali ya Sudan imeelezwa kuwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani kwa sasa, huku mapigano kati ya RSF na jeshi la serikali yakisababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na kuwalazimisha zaidi ya milioni 12 kukimbia makazi yao. Wengi wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani, huku wengine milioni 4 wakibaki kuwa wakimbizi wa ndani.
Mbali na El-Fasher, maeneo ya Kordofan na Darfur yameripotiwa kuwa na viwango vya juu vya njaa, hasa kwa familia zinazoongozwa na wanawake. Kwa mujibu wa mwakilishi wa Shirika la UN Women nchini humo, Salvator Nkurunziza, hali hiyo imewaweka wanawake na watoto katika mazingira ya hatari ya kiafya na kijamii.
"Katika idadi ya wakimbizi wa ndani milioni 5.4, asilimia 75 ya familia zinazoongozwa na wanawake zinakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula."
Wakati misaada ya kibinadamu ikizidi kupungua — ambapo ni asilimia 23 tu ya mahitaji ya ufadhili wa dola bilioni 4.16 imepatikana — mashirika ya Umoja wa Mataifa yanazidi kuililia dunia kuchukua hatua za dharura. Hata hivyo, hali ya kiusalama na mvua zinazoendelea zimekuwa kikwazo kikubwa kwa juhudi za kupeleka misaada kwa walio hatarini.
Sudan yaishtumu UAE kufadhili mamluki wa Colombia kupigana bega kwa bega na RSF
Wakati huo huo, serikali ya Sudan imeishtumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kufadhili na kutuma mamluki kutoka Colombia na baadhi ya nchi jirani barani Afrika kusaidia kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) katika vita vya ndani vinavyoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Sudan, serikali inadai kuwa ina ushahidi usiopingika kuhusu ushiriki wa mamluki hao wanaofadhiliwa na UAE, ingawa haijatoa vielelezo wazi kwa umma. Umoja wa Falme za Kiarabu na Colombia bado hawajajibu tuhuma hizo.
Tuhuma hizi zinakuja wakati ambapo UAE imekuwa ikijitokeza kama mchezaji mkubwa katika siasa za eneo la Afrika Kaskazini na Pembe ya Afrika, ikihusishwa na miradi ya kiuchumi, misaada ya kibinadamu na ushawishi wa kisiasa.
Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa usaidizi wa kijeshi wa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja unaweza kuongeza mvutano wa kikanda na kuchochea migogoro badala ya kuleta suluhu. Hii ni hasa kutokana na tabia ya RSF kuhusishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika Darfur.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wengine wanaona tuhuma hizi za Sudan dhidi ya UAE kama sehemu ya juhudi za kisiasa kugeuza mwelekeo wa lawama kutoka kwa serikali ya Sudan yenyewe, ambayo pia imekuwa ikikosolewa kwa kushindwa kulinda raia na kwa kujihusisha na vitendo vya ukatili.
Hali hii inaibua maswali kuhusu dhima ya mataifa ya Kiarabu na jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha kwamba mzozo wa Sudan haugeuki kuwa vita vya kisproxy (proxy war) vinavyochochewa kutoka nje ya mipaka ya taifa hilo.