Maelfu wajitokeza kupinga siasa kali Ujerumani
3 Februari 2025Kulingana na polisi, angalau watu 160,000 walijitokeza na kushiriki maandamano hayo.
Waandalizi wa maandamano hayo lakini wanasema watu laki mbili walishiriki kupinga kuvunjwa kwa makubaliano ambayo si ya kisheria au "ukuta wa moto" ya kutoshirikiana kwa njia yoyote ile na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Alternative für Deutschland AfD, ambayo yapo tangu mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz baada ya maandamano hayo aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba "maelfu wamejitokeza kutuma ujumbe kwamba, hakuna ushirikiano na mrengo wa siasa kali."
"Ushirikiano na shetani"
Baadhi ya waandamanaji, wamekituhumu chama cha CDUna kiongozi wake Friedrich Merz kwa kuingia kwenye ubia na "shetani" kwa kutafuta uungwaji mkono wa chama cha AfD kupitisha mswada wa kuzuia uhamiaji.
Mswada wa kutaka kuzuia uhamiaji uliokuwa umewasilishwa na mgombea ukansela wa chama cha CDU Friedrich Merz haukupitishwa bungeni Ijumaa iliyopita.
Lakini Merz ameungwa mkono na chama chake kuelekea mikutano ya kamati za vyama itakayofanyika Jumatatu huko Berlin.
Mkuu wa jimbo la Hesse Boris Rhein wa chama cha CDU pamoja na wawakilishi wengine wa chama hicho wameunga mkono sera ya Merz kuhusiana na uhamiaji.
Alipoulizwa iwapo ushirikiano wa Merz na chama cha AfD ilikuwa ni makosa, Rhein amepinga, "Hapana, ni kinyume cha hicho. Raia na wapiga kura sasa wanajua ni nani anayesimama wapi na ni yupi mwenye msimamo upi," alisema waziri mkuu huyo wa jimbo la Hesse.
Hakuna kinachofanyika kuhusu wahamiaji
Kiongozi wa chama cha CSU Markus Söder pia amemtetea Merz akiliambia shirika la habari la Ujerumani ZDF kwamba, "kura zimeongezeka pakubwa katika chama chao" na hasa kwa Merz kama mgombea wa ukansela.
Ameongeza kuwa kwa miaka mingi, raia walikuwa hawaamini kwamba lolote linafanyika ili kuzuia uhamiaji haramu. "Wiki hii muungano wetu(CDU/CSU) ulionyesha kwamba una nia," alisema Söder.
Merz kwa mara nyengine tena hapo Jumapili, aliondoa uwezekano wowote wa kuunda serikali kwa ushirikiano na chama cha AfD endapo atachaguliwa kuwa Kansela.
Tafiti za maoni zinaonyesha kuwa chama cha CDU na chama chake ndugu CSU vinaongoza kwa asilimia 30 kuelekea uchaguzi wa Februari 23 nchini Ujerumani, huku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kikiwa na asilimia 20 katika nafasi ya pili.
Vyanzo: DPAE/AFP