Maelfu waendelea kuutazama mwili wa Papa Francis
24 Aprili 2025Matangazo
Kanisa la Mtakatifu Petro limefungua milango yake tena leo baada ya kufungwa kwa muda kwa ajili ya kuwapa fursa waumini kutoka kote duniani kutoa heshima zao za mwisho kwa Papa Francis.
Mnamo Jumatano kanisa hilo lilistahili kufungwa saa sita usiku ila liliendelea kuwa wazi hadi saa kumi na moja na nusu asubuhi kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamepanga foleni kuuona mwili wa Papa Francis.
Kufikia sasa zaidi ya watu 50,000 wamekwisha toa heshima zao za mwisho kwa papa tangu mwili wake ulipowekwa katika jeneza la wazi kwa ajili ya umma kuutazama hapo jana.
Papa Francis alifariki dunia siku ya Jumatatu akiwa na umri wa miaka 88 katika makao yake huko Vatican.