Maelfu waandamana Ujerumani kupinga siasa kali
3 Februari 2025Maandamano hayo yalifanyika kufuatia hatua ya wiki iliyopita ambapo chama cha upinzani cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU, kiliposhirikiana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD na kujaribu kupitisha sheria kali dhidi ya uhamiaji.
Idadi kubwa ya watu waliandamana jana Jumapili katika mji mkuu wa Ujerumani- Berlin, ambapo idadi yao inatajwa na polisi kufikia watu 160,000 huku waandalizi wa maandamano hayo wakisema kuwa idadi hiyo ilifikia watu laki mbili ambao walijitokeza kupinga makubaliano ambayo yalishindwa hata hivyo kupitishwa na Bunge Ijumaa iliyopita.
Maandamano hayo yalilenga kupinga hatua ya ukiukaji wa chama cha Christian Democratic Union (CDU) kunako makubaliano makubwa kuwahi kushuhudiwa baada ya vita vya Pili vya Dunia kati ya vyama vya kisiasa kutoshirikiana kwa namna yoyote na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia katika ngazi ya kitaifa.
Soma pia: Muswada wa uhamiaji Ujerumani washindwa kupita bungeni
Waandamanaji hao wameishutumu CDU, ambacho ni chama kikuu cha upinzani kwa sasa nchini Ujerumani, pamoja na kiongozi wake Friedrich Merz, kwa kufanya kile walichokiita "makubaliano na shetani" kwa kutaka kuungwa mkono na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD) ili kupitisha muswada wa kupinga uhamiaji.
Baadhi ya waliohudhuria maandamano hayo walisema Kupambana na itikadi kali za mrengo wa kulia, ni muhimu.
" Ni muhimu kwangu kuonyesha kwamba demokrasia inahusisha mshikamano na nia ya kuafikiana." Mmoja wa waandamaji alisema huku mwingine akisisitiza kwamba "tunapaswa kujitenga kabisa na siasa kali za mrengo wa kulia."
Maandamano mjini Frankfurt na kauli ya Scholz
Katika mji wa Frankfurt karibu watu 9,000 walimiminika mitaani kupinga ushirikiano huo, wakiwa na mabango yanayopinga ubaguzi na kuimba nyimbo zinazomaanisha kuwa hawataki kuiona Ujerumani ikirejea kwenye enzi ya utawala wa manazi.
Maandamano hayo ambayo yalihudhuriwa na idadi kubwa ya watu kuliko ilivyotarajiwa yalizusha baadaye vurugu na makabiliano na polisi ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.
Soma pia: Maelfu wajitokeza kupinga siasa kali Ujerumani
Baada ya maandamano hayo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba "maelfu wamejitokeza kutuma ujumbe kwamba, hakuna ushirikiano wowote na mrengo wa siasa kali."
Akijaribu kujitetea, Merz amesisitiza hapo jana kuwa hakuna uwezekano wowote wa kuunda serikali kwa ushirikiano na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD endapo atachaguliwa kuwa Kansela lakini akaonyesha nia ya kuendelea kuufanyia kazi muswada huo tata na ameungwa mkono na chama chake kuelekea mikutano ya kamati za vyama itakayoanza leo mjini Berlin.
Vyama vya CDU na CSU vinaamini kuwa muswada wa uhamiaji wenye utata umeimarisha kwa kiasi kikubwa nafasi zao kabla ya uchaguzi.
Tafiti za maoni zinaonyesha kuwa chama cha CDU na kile cha CSU vinaongoza kwa asilimia 30 kuelekea uchaguzi mkuu wa Februari 23 nchini Ujerumani, huku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kikiwa katika nafasi ya pili na asilimia 20.