Maelfu kuendelea kutoa heshima ya mwisho kwa Papa Francis
24 Aprili 2025Dunia inaendelea kuomboleza kifo cha kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, aliyeaga dunia Jumatatu wiki hii akiwa na umri wa miaka 88, baada ya kuugua kwa muda mrefu. Papa Francis anatarajiwa kuzikwa Jumamosi.
Makumi ya maelfu ya watu wanatarajiwa kuendelea kujitokeza hii leo kuutazama mwili wa aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Zoezi hilo lililoanza hapo jana litaendelea hadi siku ya mazishi yake.
Asubuhi ya leo zoezi hilo litafunguliwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kuanzia majira ya saa moja asubuhi hadi saa moja jioni kwa saa za Vatican.
Soma zaidi:Maelfu wafurika kutoa heshima ya mwisho kwa Papa Francis
Hapo jana, mwili wa Papa ulibebwa kwenye jeneza lililo wazi kutoka kwenye makazi yake ya Casa Santa Marta na kupelekwa katika kanisa hilo na walinzi wanane waliongozana na maandamano, ambayo yalihudhuriwa pia na makadinali.
Duru za ndani kutoka Vatican zinakadiria kwamba kufikia jana jioni watu 20,000 hivi tayari walikuwa tayari wameshautazama mwili wa papa huku karibu watu 100,000 walikuwa wamekusanyika nje kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Maziko ya Papa Francis yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi.
Viongozi mbalimbali wa dunia wanatarajiwa kuhudhuria
Kadinali Kevin Farrell, ambaye anakaimu nafasi ya Papa hadi pale atakapochaguliwa kiongozi mpya atasimamia shughuli za kutiwa muhuri kwenye jeneza la papa mnamo siku ya Ijumaa majira ya saa mbili usiku ambapo Vatican imetangaza kwamba umati mkubwa wa watu unatarajiwa siku hiyo.
Viongozi mbalimbali wengi wa dunia watahudhuria mazishi siku ya Jumamosi, akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye atakuwa anasafiri kwa mara ya kwanza tangu arejee katika ikulu ya Marekani kwa mara ya pili.
Soma zaidi: Wakristo kote duniani wamuombea Papa Francis
Wanasiasa na wawakilishi wa kanisa hilo kutoka maeneo mbalimbali duniani kote watakuwepo kwenye misa ya mazishi kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na wengine wengi wanatarajiwa pia kushiriki misa hiyo.
Kutoka Ujerumani, Rais Frank-Walter Steinmeier na Kansela Olaf Scholz watahudhuria. Rais wa Urusi Vladimir Putin hatohudhuria mazishi hayo ingawa atawakilishwa waziri wa utamaduni Olga Lyubimova, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema hapo jana.
Usalama mjini Rome waimarishwa
Hali ya kiusalama imeimarishwa mjini Rome ambapo polisi wamesambazwa kuhakikisha usalama ingawa duru zinasema vikosi hivyo vya usalama vinakabiliwa na changamoto kubwa ya vifaa kutokana na utitiri unaotarajiwa wa waumini na wageni wengi wa kiserikali.
Baada ya sherehe za mazishi, mambo yote yatahamia shughuli ya kumtafuta Papa mpya ambayo inatarajiwa kuanza mapema mwezi Mei.
Soma zaidi: Shughuli ya umma kuutazama mwili wa papa yaanza Vatican
Makadinali 135 walio na umri wa chini ya miaka 80 wanastahili kupiga kura kwa papa mpya. Walakini, makadinali wawili wenye umri wa miaka 79 ambao ni Askofu Mkuu wa Valencia,Antonio Cañizares na Askofu Mkuu Mstaafu wa Sarajevo, Vinko Pulji wamekataa kushiriki zoezi hilo kutokana na sababu za kiafya.
Kufuatia hatua hiyo, viongozi 133 wa kanisa wana uwezekano wa kuamua hatma ya mrithi wa Papa Francis. Mchakato wa kupiga kura ni wa siri. Mchakato huo unaweza kuhitimishwa ndani ya masaa machache au kuchukua siku kadhaa, kwani hakuna kikomo cha muda.