Maduka Makubwa ya Biashara yashamiri Dar es Salaam
23 Juni 2025Soko hilo linawahudumia pia wafanyabiashara kutoka nje ya nchi ambao wanakwenda kununua bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa nchini humo na kutoka mabara mengine.
Katika siku za hivi karibuni Tanzania hususan jiji la Dar es Salaam linashuhudia ongezeko la maduka makubwa ya biashara yanayouza bidhaa mbalimbali, na baadhi ya maduka hayo ni yale yanayomilikiwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi. Ongezeko la maduka hayo makubwa ya biashara yameanza kuibua maswali, je inaashiria nini kwa uchumi wa nchi, lakini pia ipi nafasi ya bidhaa za wafanyabiashara wa ndani kuuza bidhaa zao katika maduka hayo?
Hivi karibuni duka kubwa la kibiashara lilifunguliwa katika jiji la Dar es Salaam. Duka hilo kubwa lina bidhaa za kila aina huku asilimia karibu 99 ya bidhaa zikiwa zinatoka China, na hata mwekezaji wake anatokea katika taifa hilo kinara kwa kuwa na uchumi imara duniani. Kila kona ya Dar es Salaam kwa sasa kuna maduka makubwa ya biashara, watu wengi hususan wakazi wa jiji hilo lenye watu milioni 5 wamekuwa wakijiuliza kulikoni? Na hii ina maana gani kwa uchumi wa nchi.
Maduka makubwa ya kibiashara yanasaidia kukuza ajira
Beatrice Kimaro, Mtaalamu wa Uchumi ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi, anasema uwepo wa maduka hayo makubwa ya biashara unasaidia kuchochea ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi. ''Kwa mfano kwa wastani duka moja kubwa linaweza kuwajiri kwa wastani watu 500 hadi 1,000. Hapa nazungumzia wafanya usafi, walinzi, wafanyakazi wa mule ndani na wengine wengi. Kwa hiyo unaweza kuona watu 500 hadi 1,000 wanaweza kuajiriwa kwenye jengo moja tu na hii inachochea ongezeko la ajira,'' alifafanua Kimaro.
Kulingana na mtaalamu huyo wa uchumi, kuongezeka kwa majengo hayo kunaambatana na uboreshaji wa barabara, lakini pia unasaidia huduma za umeme. Aidha, ongezeko la maduka hayo makubwa ya biashara yanatafsiri hasi katika uchumi wa nchi. Anasema biashara nyingi zinazouzwa zinajikita sana kwenye bidhaa zisizo za uzalishaji wa ndani kwa mfano nguo na vifaa vya kieletroniki na hivyo kuongeza matumizi ya fedha za kigeni kwa kuagiza bidhaa.
''Kwa mfano nitakupa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA mwaka 2023 zilionesha kuwa bidhaa za rejareja za walaji kutoka nje zilichangia zaidi ya asilimia 45 ya mauzo ya mali ya maduka makubwa hususan zinazouzwa Dar es Salaam, na ndio mana utakuta wamiliki wa majengo haya sio Watanzania na kama sio Watanzania utakuta mara nyingi bidhaa wanazouza zinatoka katika nchi zao au wanaagiza kutoka mataifa mengine,'' alibainisha Kimaro.
Kilio kikubwa cha wafanyabiashara wazawa ni kuona bidhaa zao hazipati nafasi ya kuuzwa katika maduka hayo makubwa ya biashara, hususan yale yanayomilikiwa na wenyeji. Leah Mayaya, Mkurugenzi wa kampuni ya Heaca inayoshughulika na usindikaji wa viungo vya chakula na unga wa lishe, anasema wamefika kuwafikishia bidhaa zao, lakini mwitikio wao umekuwa wa kuchelewa.
''Kwa sababu katika moja ya maduka tulipofika, walitupa vigezo kisha wakatuambia tusubiri majibu, lakini imekuwa kimya sasa ambapo ni zaidi ya miaka miwili toka tuwafikie ambapo ilikuwa 2022 na sasa ni 2025. Hivyo, nashindwa kusema moja kwa moja kwamba hawataki au vipi kwa sababu hawakusema hawachukui,'' alisema Mayaya.
Watanzania wakwama kuuza bidhaa zao katika maduka makubwa
Changamoto aliyokutana nayo Mayaya, imewakumba pia wafanyabiashara wengine wa Tanzania ambao waligonga mwamba kupata nafasi ya bidhaa zao kuuzwa katika maduka makubwa ya biashara ya wawekezaji kutoka nje ya nchi. Dokta Hildebrand Shayo mtaalamu wa uchumi na mfanyabiashara, yeye anasema kuna sababu kadhaa zinazochangia wafanyabiashara nchini Tanzania kushindwa kuuza bidhaa zao katika maduka makubwa ya biashara.
''Siku za nyuma niliwahi kufanya utafiti na kuanza kuuza ubuyu, nilitumia vifungashio vyenye ubora wa hali ya juu kama ule unaouzwa kwenye masoko pale London, Uingereza. Na kwa kweli nilifanya biashara na hapa nimezungumzia ubuyu tu, lakini bado kuna asali, pilipili hoho, tangawizi, binzari na mazao mengi tu. Kwa hiyo kuwepo kwa haya maduka makubwa ya biashara ni fursa kwa upande mmoja, lakini ni changamoto kwa upande mwingine ambao tunaacha utamaduni wa kutumia vya kwetu, tukidhani kutumia vya nje ndio bora zaidi,'' alisisitiza Dokta Shayo.
Uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuzidi kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja kunaelezwa na wataalamu wa masuala ya uchumi na biashara kuwa kutaongeza ushawishi kwa wawekezaji kuwekeza zaidi katika maduka hayo makubwa ya biashara. Wataalamu hao wa uchumi akiwemo Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Omar Mbura, wanasema suala la ushindani wa kibiashara haliepukiki kwa sasa.
''Nikiri tu kwamba ukija kuangalia kwenye ubora wa bidhaa inawezekana kabisa ukiacha uzalendo watu wengi wanapenda bidhaa kutoka nje na tafiti zinaonesha hivyo, lakini kwa upande mwingine ni kwa nini baadhi ya bidhaa kutoka nje bei zake zinaweza kuwa chini hilo nalo la kuangalia. Kimsingi watu wengi wanapenda bidhaa ambazo bei zake ni gharama nafuu tuna haja ya kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kuboresha bidhaa zetu, bei pamoja na kusambaza inavyostahili,'' alisema Professa Mbura.
Licha ya wafanyabiashara wazawa kutakiwa kuwa tayari kushindanisha ubora wa bidhaa zao na zile kutoka nje ya nchi, bado Beatrice Kimaro Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi anaamini muongozo lazima utolewa kwa wamiliki wa maduka hayo makubwa ya biashara ili wazawa waelewe kitu gani ambacho kinatakiwa.
Wafanyabiashara wadai uwazi zaidi
''Tulikuwa tunashauri zoezi hili lifanyike kwa makubaliano ya pande zote. Kwamba labda kuna vigezo au changamoto ambao wao wanaona ipo kwa wazalishaji wa Kitanzania ni vizuri wakawasiliana na sisi ili tuweze kuboresha, ila kwa kukaa kimya unashindwa kuelewa ni kwamba hawapo tayari au wana sababu. Pengine wangefunguka ingetusaidia sana. Unaweza ukadhani wapo kwa ajili ya kufanya biashara za kwao tu, wameweka uwekezaji hapa, lakini wanaleta bidhaa zao tu,'' alifafanua Kimaro.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikijipambanua kuwavutia zaidi wawekezaji kwa kile ambacho imekuwa ikieleza ni kutoa fursa zaidi za ajira hususan kwa vijana, lakini kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki. Waziri wa Viwanda na Biashara Dokta Selemani Jafo aliwahi kusema kuwa serikali itahakikisha inavilinda viwanda vya ndani.
''Naomba niwahakikishe kwamba tutajitahidi kupitia baadhi ya mambo yenye changamoto kubwa ya wazalishaji wa ndani na hasa bidhaa zinazozalishwa ndani. Tutalifanya hili kwa nguvu kubwa kuhakikisha bidhaa za ndani zinapata masoko kwa lengo la kuhakikisha tunatunza ajira na uendelevu wa viwanda vyetu,'' alibainisha Waziri Jafo.
Makala hii imeandikwa na Anuary Mkama