Madai ya Trump yasababisha mvutano kati ya India na Marekani
25 Juni 2025Kumeibuka mvutano mpya kuhusu uhusiano wa India na Marekani kufuatia madai ya Rais Donald Trump kuwa ndiye aliyefanikisha usitishaji wa mapigano kati ya India na Pakistan. Itakumbukwa kwamba mataifa hayo mawili yalitumbukia kwenye mzozo mwezi Mei mwaka huu.
Katika mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya simu, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alimwambia Rais Donald Trump kuwa hatua ya kusitisha vita ilifikiwa kupitia mazungumzo kati ya majeshi ya India na Pakistani na si chini ya usimammizi wa Marekani. Hilo limewekwa wazi na Waziri wa mambo ya kigeni wa India Vikram Misri, aliyetoa ufafanuzi baada ya mazungumzo ya Trump na Modi.
Katika taarifa yake, Misri ameeleza kuwa Waziri Mkuu Modi alisisitiza kwamba India haikukubali usuluhishi kipindi cha nyuma na kamwe haitakubali. Hakukuwa na tamko lolote la ikulu ya Marekani kuhusu suala hilo.
Modi na Trump walipangiwa ratiba ya kuonana pembezoni mwa mkutano wa kundi la nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani G7 lililofanyika Canada lakini hawakukutana kwani Trump aliondoka mapema kutokana na hali tete iliyokuwa ikiendelea Mashariki ya Kati.
Licha ya kuwa Modi na Trump wana uhusiano mzuri kuna imani kuwa kutokutabirika kwa Trump, na mbinu yake ya kuangalia zaidi maslahi ya kibiashara katika masuala yanayohusu sera za kigeni huenda yote hayo yakautia doa uhusiano wao
India na Marekani wako kwenye mazungumzo ya biashara
Kwa sasa, India inafanya mazungumzo yanayolenga kupata makubaliano ya kibiashara na Marekani lakini yamekumbana na changamoto kadhaa. Ni wakati tarehe ya mwisho ya kusitishwa kwa ushuru uliotishiwa kuwekwa na utawala waTrump dhidi ya washirika wa kibiashara wa Marekani.
Balozi wa zamani wa India kwa Pakistan Ajay Bisaria ameiambia DW kuwa hadi sasa New Delhi imekuwa ikikabiliana na Trump kwa utulivu wa kimkakati. Ameongeza kuwa pamoja na hilo baada ya Trump kudai alikuwa na jukumu kubwa katika kuusuluhisha mzozo wa hivi karibuni wa Pakistan na India, umma wa India utalisahihisha hilo. Bisaria anafafanua kuwa maoni ya watu wa India yanaonesha kuwa kwa sasa Marekani ni mshirika asiyeweza kutegemewa.
Mwanadiplomasia huyo wa India anaongeza kuwa kila wakati Marekani inapojihusisha na jeshi la Pakistan, kama wakati Trump aliposhiriki chakula cha mchana na mkuu wa jeshi la taifa hilo Jenerali Asim Munir, huwa ni ishara mbaya.
India inaishutumu Pakistan kwa kuwasaidia magaidi
Ieleweke kuwa, India inaishutumu Pakistan kwa kuunga mkono ugaidi katika eneo la mpaka baada ya shambulio dhidi ya raia lililowauwa watu 26 katika eneo la Kashmir lililo chini ya India. New Delhi iliilaumu Islamabad kwa kusaidia kufanikisha shambulio hilo suala ambalo Pakistan inalikanusha
Kwa upande wake Meera Shankar, aliyewahi kuwa mjumbe maalumu wa India kwa Marekani ameiambia DW kuwa ni vigumu kupinga madai ya Trump kuwa alisaidia kuumaliza mzozo wa India na Pakistan kwani India haikutaka kuingia katika vita kamili. Anasema inawezekana kuwa utawala wa Trump ulisaidia kuishawishi Pakistan kuachana na mapigano.
Mkuu wa shule ya masuala ya kimataifa katika chuo kikuu cha Jawaharlal Nehru University cha New Delhi Amitabh Mattoo, amesema kuwa yanayoendelea sasa kati ya Marekani na India yameonesha msuguano mpya na kukosa uaminifu katika uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, lakini ushirika unaweza kuzishinda changamoto na kutengeneza mustakabali bora zaidi wa kudumu na kutoa fursa mpya.