Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo:
16 Desemba 2003Kuhusu mafanikio kwenye tume ya upatanishi katika bunge mjini Berlin, gazeti la STUTTGARTER NACHERICHTEN linasema: mapatano hayo hayaonyeshi dhahiri ni upande gani ulioshinda wala ni nani aliyeshindwa. Kwani kile kinachodhamiriwa na serikali pamoja na upande wa upinzani, kinaihusu Ujerumani kwa jumla. Hata mapatano yaliyoafikiwa kuhusu mageuzi ya huduma za kijamii, hayairejeshi Ujerumani katika mkondo wa mafanikio. Hata hivyo, mapatano hayo huenda yatachangia kusimamisha hali ya kuzidi kukwama kwa maendeleo. Vyama vyote vya kisiasa vimeshuhudia kwamba, vina hamu na uwezo wa kutenga kando masilahi yao na badala yake kutafuta kwa pamoja mikakati ya kulitatua swala hili la mageuzi. Hata ikiwa haukufikiwa umbali mkubwa ambao ungekuzwa bora, mwanzo wake umeshaanzishwa, hatua nyingine zitafuata.
Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri kimataifa, DIE WELT, linaandika: Kimetokea kile ambacho hakikutakiwa kitokee. Kwa munda wa miezi kadhaa, wanasiasa wa upande wa kushoto na wa upande wa kulia, wamekuwa wakitoa mashauri chungu nzima ya kuurekebisha mpango wa mageuzi wa serikali. Isitoshe, kwa muda wa miezi kadhaa, yamekuwa yakipaazwa matumaini ya kukutikana kifurushi cha upunguzaji kodi, chini ya mit wa Krismasi. Lakini kifurushi hicho hakikujaa mapendekezo ya kutosha. Siasa za Ujerumani zimechelewa kutumia fursa muafaka, ya kuwafanya raia kuamini siasa za serikali - kwa maneno mengine masikitiko makubwa badala ya shangwe.
Nalo gazeti la mji wa kusini mwa Ujerumani Munich, SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linatoa maoni kwamba: Kile kinachobakia sasa ni Knasela kuwa na matumaini mnamo miezi ijayo. Endapo yatapatikana masharti ya kukwamua maendeleo ya kiuchumi, basi atajaribu kuthibitisha tena kwenye tume ya upatanishi kwamba, mikakati yake inazingatia faida ya dola. Lakini endapo hali ya ustawi wa kiuchumi haitafufuka tena, mzozano katika serikali utaendelea, mapato kutokana na kodi yatapungua na kiwango cha madeni kitazidi kupanda. Vyama vya upinzani vinaelemea upande ambao hauwezi kuvihatarisha. Iwapo hali ya ustawi wa kiuchumi itaboreka, basi upande huu utasema ndio uliopelekea kufanikiwa kwa mapatano hayo. Lakini iwapo hali itakuwa kinyume chake, basi upande wa upinzani utasema, haukuzuwia mpango huo wa serikali, Kansela ndiye atakayelaumiwa kwa kila kitu. Gazeti la hapa mjini Bonn, GENERAL- ANZEIGER, kuhusu mada hii linasema: Mapatano haya ambayo yalipatikana kwa shida yanashuhudia jinsi Ujerumani inavyojitatiza yenyewe. Ni hali isiyovumilika kwamba, mshindi kwenye uchaguzi mkuu anayaweka maamuzi yote katika ushirikiano na wale walioshindwa kwenye nuchaguzi huo. Je, nani aliye ni serikali na ninani aliye ni mpinzani wake? Hapa kinahitajika kipaji cha kutatua swala hili kati ya wanasiasa wa serikali kuu na wa serikali za mikoa, kwani cha mstari wa mbele ni masilahi ya mageuzi na ya demokrasia. Masilahi haya yanabidi kuwapa nafasi wapigaji kura, ya kufahamu kinaganaga siasa za serikali, yaani ni nani anayebeba dhamana ya mafanikio au ya kukwamisha maendeleo.
Gazetui la mji mkuu BERLINER KURIER, linazingatia hali nchini Irak, baada ya kukamatwa dikteta wa zamani Saddam Hussein, kwa kuandika: Tunaona picha za pango la kimaskini, ambalo kuta zake zinaloweka na chini yake kitanda cha bao. Picha za mtu ambaye hakukoga tangu muda mrefu na mwenye mandevu marefu. Saddam alivutwa bila ya upinzani kutoka shimo lake ardhini. Picha hizi kwa kweli zinamfanya mtu kumhurumia. Lakini picha hizi zizimfanye mtu kusahau kwamba, mtu huyu alikuwa ni dikteta na muuaji katili. Sasa amepoteza makasri yake ya anasa na hata heshima yake ya kiutu.
Gazeti la OBER-PFÄLSER NACHRICHTEN, linakamilisha mada hii kwa kuandika: Kwa bahati mbaya hakuna kundi lenye uwezo wa kuongoza wakati huu nchini Irak. Kinyume chake, nchi hiyo inakabiliana na hali ya utengano kati ya wasuni, washia na wakurdi, wanasiasa waliokuwa uhamishoni na wale waliosalia nchini. Hapaonekani ni nani angekuwa na kipaji cha kushikia usukani uongozi. Kwa sababu hali hii ya kutatanisha, nchi hii kwa kweli inahitaji uongozi madhubuti na wa kuaminika. Wamerikani wamepiga hatua mojawapo kubwa ya mafanikio, lakini mustakabali wa kisiasa wa Irak bado haujulikani.