Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo
12 Februari 2004Mfumo wa sasa wa huduma za wastaafu, unaelekea umeshakwama, kwa sababu unaelemea upande mmoja tu. Kwani endapo viwango vya kazi anayofanya mtu vya kugharamia mpangho huo vitapungua, hapana shaka mfumo huu hautakuwa na maana tena. Kwa maneno mengine, wale wanaopata mishahara midogo watapatwa na hasara ya kupoteza michango yao. Ikiwa wana bahati, wastaafu walioingia katika maisha ya uzeeni, watakuwa wakipatiwa kiasi ya Euro chache tu zaidi, kupita mfanya kazi ambaye hakuwahi kuchangia hata hela moja. Lakini yule ambaye anataka kuendelea kunufaika na mfumo mpya, basi atabidi kuchangia zaidi kupita kiwango cha kumwezesha kukidhi mahitaji yake ya maisha. Gazeti mashuhuri la shuguli za kibiashara, HANDDESLBLATT, kuhusu mada hii linasema: Alao tangu mjadala wa jana bungeni kuhusu mapendekezo mapya ya kuchangia mpango wa mageuzi wa serikali, inajulikana wazi: wimbi jipya la matatizo halitaweza kuzuilika. Katika jamii ambapo idadi ya wastaafu inazidi kupanda mfululizo, lakini katika upande wa pili ambapo maelekeo ya kubuni nafasi za ajira na ustawi wa uchumi yanaendelea kudidimia, wastaafu hawawezi kujiokoa na mpango huo wa mageuzi. Na ikiwa waajiriwa, viongozi wa uchumi na walipaji kodi hawatakuwa na pesa za kugharamia mpango huo, basi panazuka haja ya kufuatwa mojawapo ya njia mbili: Njia mojawapo ni ama wastaafu kuwa tayari kugharamia binafsi huduma zao za uzeeni, au umri wa kumwezesha mstaafu kisheria kuingia katika maisha ya uzeeni utabidi kupandishwa.
Gazeti mashuhuri la hapa jijini Bonn, GENERAL ANZEIGER, linatilia uzito mashambulio mfululizo ya kujitoa mhanga nchini Irak kwa kuandika: Kwa wale walioko nyuma ya mashambulio hayo, halikadhalika wanakabiliwa na matatizo. Kwani ijapokuwa lengo la mashambulio hayo ni kudhoofisha nguvu za wanajeshi wa wakaliaji, wale wanaofanya mashambulio hayo wanajifanya kukabiliwa binafsi na hatari ya kutengwa na raia wenzi wao nchini. Hali hii inaeleweka kwa sababu mamia ya raia wanaofariki kila kukicha, hayawezi kuhalalisha vitendo vya umwagaji damu. Gazeti la FRANKENPOST, nalo linasema linajua ni akina nani walioko nyuma ya mashambulio hayo ya kila siku, linapoandika: Kila kukicha zinasikika fununu za utando wa Al-Qaida kuhusika kwa kushirikiana pamoja na wale nchini Irak, ambao hawako taari kusalimu amri na kuisahau kabisa enzi ya dikteta wao wa zamani Saddam. Na sababu zake zinaonekana dhahri, nazo ni jaribio la kuchochewa vita vya kiraia nchini humo. Gazeti lingine mashuhuri la kusini mwa Ujerumani, SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, katika uhariri wake linazingatia yale mafanikio ambayo mgombea wadhifa wa rais nchini Marekani, John Kerry, anajipatia mfululizo kwenye uchaguzi mdogo hadi sasa, kwa kuandika: Wale wanaoshangilia tayari ushindi huu kutoka kambi ya kushoto, wanabidi kuonywa kwamba, hata John Kerry si masiya ambaye angedhubutu kuielekeza marekani katika upande wa social-demokratik. Kwa mtazamo wa kiulaya, Kerry ni mtu ambaye ana kipaji cha kuwavutia raia wengi nchini mwake Marekani. Na kama ilivyotokea kwenye mchuano kati ya George W.Bush na rais wa zamani Bill Clinton mwaka 1992, itazuka hali inayofanana pia katika mwaka huu. Rais aliyeko madarakani, anaweza kushindwa tu, iwapo anajihatarisha binafsi. George W. Bush anajitahidi kwa kila njia kujihakikishia duru ya pili ya kushikilia wadhifa huu wa rais. Tunakamilisha uchambuzi wa uhariri wa magezeti ya Ujerumani hii leo, kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la mji wa Karsruhe, BADISCHEN NEUSTEN NACHERICHTEN, kuhusu mada hii, linaandika: Hata ikiwa uamuzi wa mwisho wa kumtangaza Kerry kuwa mgombea rasmi wa wadhifa wa rais dhidi ya rais Bush, bado haujapatikana, tayari kuna taarifa ya kuwafurahisha wanachama na wafuasi wa chama cha demokratik: Nayo ni kwamba, kampeni zake kwenye uchaguzi mdogo, zimewashawishi raia wengi wa kawaida, hasa kuhusiana na takwa lao la dhati la kumpokonya Bush duru ya pili ya Urais. Kwa veterani huyu wa kivita Kerry, inaelekea chama cha kidemokrasi kipegundua mtu ambaye ana kipaji cha kupatanisha safu mbali mbali za kijamii, pamoja na kufahamu hisia za Wamerikani baada ya mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11 septemba.