Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo:
17 Februari 2004Gazeti mashuhuri la mashariki mwa Ujerumani, LEIPZIGER VOLKSZEITUNG, linapozingatia msimamo wa kiongozi wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, wa kukataa ushirika wa aina maalum pamoja na umoja wa ulaya, linaandika: Inafahamika ni kwanini kiongozi wa Uturuki Erdogan anakatalia mbali ushirika wa aina hii, kwa kuuliza, je, ni nani anayeweza kula mkate mkavu wakati kuna nyama tamu ya kondoo? Sababu yake nyingine ni kwa kuwa Kansela Gerhard Schröder, ambaye anaunga mkono uwanachama wa Uturuki, atakwenda karibuni kuizuru nchi hiyo.Sababu mojawapo ya ziara yake ni kwa kuwa, serikali ya Erdogan inaonyesha utayarifu mkubwa wa kutekeleza mpango wa mageuzi, ambao unabidi kuungwa mkono kwa kila njia.
Kuchanganyishwa Uturuki na jamii za nchi za magharibi, ni masilahi ya dhati na ya tangu muda mrefu ya nchi za ulaya kwa jumla. Lakini kabla ya kupitishwa uamuzi jinsi ushirika huo ungalivyoonekana inabidi kusubiriwa hadi pale umoja wa ulaya utakapojirekebisha kamili mfumo wake.
Mada hii pia inachambuliwa na gazeti mashuhuri la biashara la mji wa magharibi mwa Düsseldorf, HANDELSBLATT, linapoandika: Muhimu saa hii kwa Erdogan, ni kuthibitisha namna anavyoweza kuaminiwa pindi aweze kupata msaada kwa malengo ya serikali yake. Labda ataweza kufanya hivyo wiki moja baada ya mwenyekiti wa chama cha upinzani CDU Angela Merkel kuizuru Uturiki, wakati atakapompokelea Kansela Schröder, ambaye anakariri mara nyingi umuhimu wa uanachama wa Uturuki katika umoja wa ulaya. Erdogan anaweza kutarajia mshikamano wa Kansela Schröder, kwa namna sawa anavyotarajia mshikamano pia kutoka nchi nyingine 25 zilizo wanachama wa umoja huu. Lakini Haja ya Uturuki inaweza kutekelezeka tu, iwapo inaungwa mkono kwa kauli ya pamoja ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.
Kuhusu uchaguzi ujao wa bunge la Ulaya, uwanachama wa Uturuki ni mada mojawapo ya safu za mbele ya nchi wanachama wa umoja wa ulaya. Kuhusu hayo gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linaandika: Kwenye uchaguzi huo wa bunge la ulaya mwezi juni, cha mstari wa mbele hakitakuwa ni kama Uturuki itaweza kushirikishwa katika umoja wa ulaya au la. Yule anayenuwia kutafuta mtafaruku katika maswala ya siasa za ndani na za nje, ataupata, kwa sababu hapa tunakabiliana na tatizo gumu kweli kutatua la siasa za nje mnamo siku za usoni. Kuifungulia au kuifungia milango Uturuki, yote yanategemea uzito wa maoni ya kisiasa ya nchi wanachama wa umoja wa ulaya.
Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani, KIELER NACHRICHTEN, linajishugulisha na mada nyingine kabisa, nayo ni jinsi serikali ya Ujerumani inavyonata katika mpango wake wa wagonjwa kudaiwa malipo maalum wanapokwenda kuonana na madaktari. Linaandika: Dai hili haliwezi kutazamwa kama ni mafanikio katika mpango wa mageuzi wa serikali. ´
Sababu ni kwa kuwa mageuzi ya huduma za afya hayakuweza kutekelezeka tangu kabla ya siku kuu za Kristmasi, bali badala yake yalifanyiwa matibabu hafifu tu ya kuwatuliza wale raia wasioridhika na mpango huo wa serikali.
Kila raia anahangaika anapojua kwamba, huenda ikawa siku moja atakuwa akiumwa, na inambidi kwenda kuonana na daktari wake. Sababu kuu ni kwa kuwa raia wengi wanashindwa kulipa kiwango hicho maalum cha kama Euro 10.
Tunakamilishiwa uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, kwa kutazama yale yanayozingatiwa na gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT, linapoandika kuhusu mada hii: Ni kweli mfumo mzima wa huduma za afya unabidi kuboreshwa, lakini sio kwa kuwataka raia kugharamia kiwango hicho maalum cha kuonana na daktari. Ushuhuda wa hayo umeshaonekana tayari, kwani idadi ya wagonjwa wanaokenda kuonana na daktari, imepungua sana. Muhimu sasa ni serikali kukaza siasa zake katika kuutekeleza mpango wake wa mageuzi haya ya afya na mengineyo ya huduma za kijmii, pia kwa nia ya kuwaridhisha wapigaji kura.