Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo
26 Februari 2004Kuhusu maadhimisho ya Jumatano ya Majivu hiyo jana katika Ujerumani, gazeti la mji wa kaskazini wa Rostock, OSTSEE-ZEITUING linaandika: Kwa mara nyingine, haya yalikuwa ni maadhimisho yaliyojaa kila kitu kwa kila mtu, kwa ufupi sherehe na hotuba za upinzani wa kisiasa. Si ajabu basi kwamba, mwenyekiti wa chama kimojawapo cha upinzani CSU na waziri mkuu wa mkoa wa kusini wa Bavaria, Edmund Sdtoiber, alishangiliwa na wengi alipopinga vikali uwanachama wa Uturuki katika umoja wa ulaya. Matamshi yake yanadokeza kwamba, swala hili kuhusu Uturuki, litakuwa mada mojawapo muhimu kwenye kampemni za uchaguzi mkuu ujao za vyama-ndugu vya CDU na CSU. Hata hivyo, hotuba za wakati wa maadhimisho haya ya Kwarisma, yanawafanya wengi kutafakari juu ya hatima ya nchi yao.
Mada hii pia inazingatiwa na gazeti mashuhuri la biashara HANDELSBLATT, kwa linaposisitiza: Hotuba zilizotolewa na wanasiasa iwe ni katika miji ya Pasaau, Biberach, Vilshofen, Düsseldorf au Demin, zinadokeza jinsi raia wengi walivyokatishwa tamaa na mikakati ya wanasiasa wengi. Kwa maneno mengine mtu anaweza kusema raia wengi kisiasa hawaamini tena viongozi wao. Wanakata tamaa hasa kwa sababu wanatambua kwamba, wanasiasa wengi wawe jijini Berlin au kwengineko, wanashindwa kusuluhisha matatizo yanayowakabili wakati huu.
Kuhusu ziara ya Kansela wa Ujerumani nchini Marekani ijumaa ijayo, yaani keshokutwa, gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG linakumbusha: Miezi michache tu iliyopita, rais wa marekani George W.Bush, alisema asingekuwa tayari kukutana ana kwa ana na Kansela Schröder. Naam, na sasa? Mambo yamemgeukia na atakuwa tayari kukutana naye. Kwani rais Bush ametambua ndiye binafsi aliyezusha msiba wa vita vya Irak, ambao hawezi kuutatua bila ya msaada wa nchi za ulaya, ikiwemo Ujerumani. Hata hivyo, inambidi Kansela kutosahau kwamba, shukuran kwa hali hii mpya , ni Marekani kushindwa kuchagua moja kati ya hali mbili mbaya.
Nalo gazeti la mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Gera OSTTHÜRINGER ZEITUNG, kuhusu mada hii linatabiri: Wakati Kansela atakapolakiwa kwa mara ya kwanza baada ya vita vya Irak na rais Bush katika Ikulu hiyo kesho, mtu hawezi kuzungumzia juu ya urafiki kati ya wanaume wawili, kwa sababu mkutano huo unatiwa dosari na misimamo iliyohitilafiana kuhusu vita hivyo. Inaelewaka pia kwa sababu viongozi hawa wawili wanashikilia misimamo inayohitilafiana sana katika baadhi ya maswala muhimu ya kimataifa. Lakini hii ndiyo sababu kwanini Kansela Schröder na Rais Bush wanataka kujaribu kujongeleana kirafiki. Rais Bush anajua barabara kwamba, angeweza kufanikiwa tu kwenye uchaguzi ujao wa rais, iwapo anazingatia kinaganaga maswala ya siasa zake za nje na za ndani. Na kwa Kansaela binafsi , ambaye wakati huu anakabiliwa na matatizo ya siasa za ndani, hii itakuwa nafasi muafaka kwake kupanda katika jukwaa la kimataifa. Gazeti mashuhuri la Kolon, KÖLNER STADT ANZEIGER, linatukamilishia uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, kwa yale linayoandika kuhusu mada hii, linapokumbusha: Ujerumani pamoja na Marekani, zinatengaza zaidi kuliko kujongeleana kishirika. I Inaweza ikawa kuna baadhi ya maswala yanayozifunganisha, lakini madola haya yanahitilafiana katika maswala kama yale ya mitazamo yao kuhusu hali na hatima ya binadamu duniani. Wakati Ujerumani inaposadiki hali na hatima hii ingeweza kutatuliwa kwa msaada wa mashirika ya kimataifa, Marekani inasadiki katika utatuzi wa kitaifa. Na wakati wajerumani wanapofuata mkondo kati ya ubepari na siasa za huduma za kijamii, wamerikani wanaamini nguvu za kibiashara duniani. Ujerumani ni dola lisilotegemea misingi ya kidini, wakati Marekani hufuata kinyume chake. Na wakati wengi miongoni mwa raia wa Ujerumani, wanapopendelea mikakati ya udumishaji amani, wamerikani huvitazama vita kama ni chombo kinachofaa katika kudumisha amani duniani. Ndio maana wakati umesshawadia wa kutafutwa na kutajwa wazi hitilafu zilizoko katika mahusiano kati ya Ujerumani na Marekani.