MADA KUU ZA WAHARIRI WA MAGAZETI YA LEO YA UJERUMANI NI: MAGEUZI KATIKA HAKI NA FURSA ZA WATUMISHI SERIKALINI NA UAMUZI WA UJERUMANI KUIPA IRAQ MAGARI YA AINA YA AINA YA VIFARU
5 Oktoba 2004Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo umetuwama juu ya haki na fursa nono za watumishi serikalini,mapendekezo ya chama kikuu cha Upinzani cha CDU ya kugeuza mfumo wa bima ya jamii na mpango wa serikali ya Ujerumani wa kuipa Irak magari ya vifaru .
Mpango ulioafikiwa na waziri wa ndani Otto Schily, Shirikisho la vyama vya wafanyikazi VERDI pamoja na shirika la watumishi serikalini kurekebisha haki za watumishi hao yamekaribishwa mno na gazeti la STUTTGARTER NÄCHRICHTEN nalo laandika:
"Unaweza kuwaamini kila kitu watumishi serikalini na waakilishi wao isipokuwa tu sio kuwa tayari kusamehe fursa nono wanazopata.Lakini, wakati sasa umewadia wanabidi kuzisamehe.Mageuzi yaliopangwa kufanywa yaweza kuwa ya juu juu tu.Lakini masharti ya kuleta mageuzi yoyote kwanza ni kufungua mlango wazi kabisa na halafu kuanza kuzifuta fursa hizo.Endapo watumishi hao wa serikali wakijiwinda kun’gan’gania fursa zao hizo nono,watakuwa wanajichimbia kaburi la kujakuwazika wenyewe.Na hatari hii ipo kweli."-laandika STUTTGARTER NARCHRICHTEN.
Gazeti la GENERAL-ANZEIGER linalotoka mjini Bonn halikuridhika hivyo na laandika:
"Kwa wale wanaopigania makuu,mwongozo wa mapendekezo ya mageuzi ya haki za watumishi serikalini ni wa kuvunja moyo.Hakuna kilicho fafanuliwa wazi: ni majukumu gani watumishi serikalini wanapaswa bado kuyatimiza,hawajazungumzia kabisa kukatazwa kwao kugoma na serikali za mikoa hazikuachiwa dhamana ya kuamua juu ya mishahara yao.Maafikiano yaliofikiwa unaweza kusema ni sawa na mapinduzi madogo katika vita vya kufuta haki na fursa zao."hilo lilikua GENERAL-ANZEIGER kutoka Bonn.
Ama gazeti la WESTFÄLISCHE ANZEIGER kutoka mji wa Hamm linaona haki na fursa za wanaohudumia idara za serikali,zisiguswe:Laandika:
"Wanasiasa wajizuwie na shauku ya kutaka kuupuuza mkono walionyoshewa na watumishi serikalini kurekebisha mambo kidogo.Kwani dharau kama hizo ndizo zinazomfanya mtumishi kuonekana kama tumjuavyo katika vikatuni."
Gazeti la KIELER NACHRICHTEN lina maoni tofauti-laandika:
"Ingelifanikiwa kuleta hali ya malipo ya haki kwa watumishi, laiti muundo wa shirikisho hautafika umbali wa kuamua haki za watumishi serikalini kuwa jukumu la serikali za mikoa.Kuchukua hatua kama hiyo ni kutoa buriani kwa mfumo wa malipo sawa kote nchini kwa watumishi milioni 1.7 wanaotumikia serikali ya shirikisho, za mikoa na wilaya. Kwa maridhiano na vyama vya wafanyikazi wapaswa watunge mfumo wa kisasa kabisa wa haki na fursa za watumishi serikalini." hilo lilikua KIELER NACHRICHTEN.
Mwongozo wa mageuzi wa chama kikuu cha upinzani CDU haukupokewa vyema alao na gazeti linalotoka Rostock: OSTSEE-ZEITUNG.Gazeti laandika:
"Uongozi wa chama cha CDU katika juhudi zake ulizopitisha tena kwa taabau, umeibuka na kitu tofauti kabisa na azma ya serikali ya vyama-tawala vya SPD na KIJANI ilivyopanga kupendekeza.Chama cha CDU kimeibuka na biramu la uliberali mambo-leo na nadharia za kiuchumi.Swali hasa :jinsi gani uchumi unaozingatia hali za wanyonge katika jamii-made in Germany- katika enzi hizi za utandawazi ungepaswa uwe, mwenyekiti wa chama Bibi Merkel na wenzake hakuweza kulijibu."Hayo ni maoni ya Ostsee Zeitung.
Likitugeuzia mada,gazeti la NORDKURIER kutoka Brandenburg,linauchambua uamuzi wa serikali ya Ujerumani wa kuipa Irak magari ya aina ya vifaru ya usafiri:
laandika:
"Serikali ya muungano wa vyama vya SPD na KIJANI ilipaswa kusimama wima na kushikilia uzi wake ule ule wa kutojiingiza katika janga la vita vya Irak na sio kuitikia mbinyo wa Marekani wa kushinikiza kuchangia kijeshi kwa nguvunchini Iraq."
Nalo likitumalizia uchambuzi huu, gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG laandika:
"Serikali inashikilia magari hayo ya usafiri hayakupangwa kutumika katika vitani nchini Iraq."Gazeti lauliza, "Ikiwa si kwanza yatatumika kwa mafunzo halafu kuwalinda wanajeshi wa Irak,magari hayo yanapelekwa Irak kwa madhumuni gani ?.