Macron: Kutambua utaifa wa Palestina ni njia pekee ya amani
9 Julai 2025Rais Emmanuel Macron ameanza ziara hiyo ya kwanza kufanywa na mkuu wa nchi ya Umoja wa Ulaya tangu Uingereza ilipojiondoa katika umoja huo.
Mfalme Charles III amemkaribisha kiongozi huyo wa Ufaransa na wote wawili wamepongeza umuhimu wa uhusiano wa mataifa hayo mawili.
Mfalme Charles alitumia hotuba yake kwa wageni wapatao 160 na washiriki wengine wa familia ya kifalme kuonya kwamba nchi zote mbili zinakabiliwa na vitisho vigumu vikubwa vinavyotoka kwenye pande mbalimbali duniani.
Katika matamshi yake ya awali katika hotuba yake bungeni, Macron nae alizungumza maneno sawa na hayo akisema kwamba nchi hizo mbili lazima zishirikiane kutetea na kufuata misingi na taratibu za kimataifa zilizowekwa baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia.
Katika hotuba yake ya muda wa nusu saa, Rais Macron amesisitiza kwamba Uingereza na Ufaransa ni lazima kwa mara nyingine tena ziuonyeshe ulimwengu kwamba muungano baina yao unaweza kuleta mabadiliko yote makubwa duniani.
Macron: Taifa la Palestina litambuliwe
Katika hotuba hiyo kiongozi huyo amegusia masuala mengine kuanzia mizozo ya kimataifa hadi suala la uhamiaji usio wa kawaida, Rais Macron amesema kwamba nchi za ulaya "hazitaiacha Ukraine" katika vita vyake na Urusi, na akatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano bila masharti huko Gaza.
Macron ameitumia hotuba yake hiyo kuitolea mwito Uingereza kwamba iungane na Ufaransa katika kulitambua taifa la Palestina, na kuweka wazi kwamba hiyo ndiyo "njia pekee ya amani" ukanda huo wa mashariki ya kati unaokabiliwa na vita kati ya Israel na Hamas.
Hii leo Jumatano, Rais huyo wa Ufaransa atafanya mikutano kadhaa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.
Itakukumbukwa kwamba baada ya kuchukua mamlaka mnamo 2024, Waziri Mkuu huyo wa Uingereza amekuwa akipambana na kutimiza ahadi yake ya kurejesha uhusiano na mataifa ya Umoja wa Ulaya kufuatia miaka mingi ya mivutano iliyochochewa na kujiondoa kwao katika umoja huo wa ulaya.
Majadiliano yao yanatarajiwa kulenga misaada zaidi kwa Ukraine iliyoharibiwa na vita na kuimarisha matumizi ya ulinzi, pamoja na juhudi za pamoja za kuwazuia wahamiaji kuvuka ujia wa bahari kwa boti ndogo suala ambalo ni lenye nguvu la kisiasa nchini Uingereza.
Uingereza kwa miaka mingi imekuwa ikiishinikiza Ufaransa kudhibiti na kusimamisha boti zinazoondoka kutoka kwenye fukwe zake zilizopo upande wa kaskazini mwa Ufaransa ili kuzuia uhamiaji.
Lakini Macron hapo jana alisema kwamba jukumu hilo ni mzigo kwa nchi zote mbili na akisisitiza kwamba lipo hitaji la ushirikiano wa dhati baina ya Ufaransa na Uingereza ili kulifanikisha hilo.
Mengi yatajadiliwa katika mkutano huo
Mbali na hilo ziara hiyo pia inalenga kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Ratiba ya hii leo ni kwamba Rais Macron atakuwa na chakula cha mchana na Starmer kabla ya viongozi hao wawili kuandaa Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Ufaransa na Uingereza hapo kesho Alhamisi ambapo wamepanga kujadili fursa za kuimarisha uhusiano wa ulinzi.
Uingereza na Ufaransa zinaongoza mazungumzo kati ya muungano wa mataifa 30 kuhusu jinsi ya kuunga mkono uwezekano wa kusitisha mapigano nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kupeleka vikosi vya kulinda amani.
Watazungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, kwa mujibu wa ofisi ya raisi ya Ufaransa.